Sunday , 7 July 2024
Home Habari Mchanganyiko Wabunge nao wataka Spika ang’oke
Habari MchanganyikoHabari za SiasaKimataifa

Wabunge nao wataka Spika ang’oke

Spika wa Bunge la Kenya, Moses Wetang’ula
Spread the love

SPIKA wa Bunge la Kitaifa nchini Kenya, Moses Wetang’ula, amekalia kiti cha moto baada ya baadhi ya wabunge kumtaka ang’atuke kutokana na mtindo wake wa uongozi kudaiwa kuwa wa ubaguzi. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Hayo yanajiri wakati vijana wa Gen Z wakiendeleza maandamano ya kumtaka Rais wa taifa hilo la Afrika Mashariki naye kung’oka madarakani kutokana na kile wanachodai kutowasikiliza na kuwarundikia kodi katika bidhaa muhimu.

Wabunge wanaotaka Spika ajiuzulu wametajwa kuwa anatoka katika Muungano wa Kenya Kwanza Alliance, hususan chama cha Rais Ruto cha United Democratic Party (UDA) ambacho kinamtaka Spika ambaye ni kiongozi wa wengi bungeni hapo kujiuzulu kwa kuwa chombo hicho kimepoteza hadhi yake.

Wabunge hao wanahoji kuwa matukio yaliyofuatia baada ya kura iliyopigwa Jumanne iliyopita kuhusu kusomwa kwa mara ya pili kwa Muswada wa Fedha, yanaashiria kuzorota kwa uhusiano kati ya Spika na wabunge, hali inayovurugwa zaidi na mtindo wake wa kuongoza Bunge la Kitaifa.

Mbunge Maalum ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha za Umma (PAC) John Mbadi amemtaja Wetang’ula kama kiini cha matatizo yanayoandama Bunge akimshutumu kwa kuua mjadala na ubaguzi.

“Hatuna tena mjadala bora jinsi ilivyokuwa hata katika enzi za chama kimoja kuanzia 1992. Chini ya Spika Francis Ole Kaparo 1992, 1997 na 2002, wabunge walipata fursa sawa ya kusikika kwenye mjadala Bungeni ikiwemo wanaopinga,” alisimulia mbunge huyo wa zamani, Suba Kusini.

Mbunge wa Kitui Mashinani, David Mwikali, ametoa wito kwa Rais kuwatimua viongozi wa Bunge akianza na Spika na viongozi wa wengi.

“Matukio yanayojiri Bungeni yanathibitisha kuwa Wakenya wamepoteza imani na waliowachagua. Kambi ya walio wachache ulielemewa na walio wengi lakini watu wametuonyesha vinginevyo,” alisema Mboni.

Seneta wa Kaunti ya Nandi, Samson Cherargei, vilevile ameashiria kuwa Spika amefeli kuliongoza Bunge kama mwenyekiti wa Tume ya Huduma ya Bunge (PSC) na ni mwepesi kuwanyamazisha wabunge wanaozua maswali.

Kifungu 106 cha Katiba ya Kenya kuhusu Spika na Manaibu wa Spika Bungeni kinatoa mwongozo kuhusu uchaguzi na utimuaji kuambatana na Kanuni za Bunge la Kitaifa.

“Ofisi ya Spika au Naibu Spika itasalia tupu – ikiwa Bunge husika litaafikiana kwa pamoja likiungwa mkono na kura za angalau theluthi mbili ya wanachama wake,” inaeleza sehemu cha kifungu 106.

Baadhi ya viongozi hasa katoka Kenya Kwanza waliochelea kutajwa vilevile walielezea kutoridhishwa kwao na matukio ya Jumanne huku wakishutumu viongozi kwa kujipiga kifua na ukaidi.

Mbali na Wetang’ula, wabunge wanataka kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wah na Kiranja wa wengi Silvanus Osoro watimuliwe.

Ingawa uvamizi wa Bunge na waandamanaji Jumanne dhidi ya Muswada wa Fedha 2024 ulizidisha maswahibu ya Wetang’ula, matatizo yake yalianza mwanzoni mwa Bunge la 13 wakati muungano wa Azimio la Umoja ulitofautiana na uamuzi wake uliotangaza Kenya Kwanza kuwa na idadi kubwa ya wabunge.

Wabunge wa Azimio nao walitoa maoni yao nje ya Bunge kwa kumshutumu Wetang’ula kwa ‘udikteta’.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Serikali yakanusha kuchelewa kutoa vibali vya uagizaji wa sukari

Spread the loveBODI ya Sukari Tanzania imekanusha taarifa za kuchelewa kutoa vibali...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Uamuzi wa serikali kuwapa wafanyabiashara vibali vya uagizaji kulishusha bei ya sukari

Spread the loveUamuzi wa Serikali ya Tanzania kutoa vibali vya uagizaji wa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

TAWA yakaribisha Watanzania, wageni kuwekeza kwenye sekta ya utalii nchini

Spread the loveMAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) iimetoa wito kwa...

error: Content is protected !!