Sunday , 30 June 2024
Home Habari Mchanganyiko Muarobaini migongano ya binadamu wanyamapori watajwa
Habari Mchanganyiko

Muarobaini migongano ya binadamu wanyamapori watajwa

Spread the love

IMEELEZWA kuwa iwapo serikali itawekeza kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi, migongano baina ya binadamu na wanyamapori chini itapungua kama sio kuisha kabisa. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Hayo yameelezwa leo Alhamisi na Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Dk Stephen Nindi wakati wa mdahalo ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) na kufadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Ujerumani (GIZ) linalotekeleza Mradi wa Kutatua Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori katika Ukanda wa Ruvuma.                                    


Dk Nindi amesema kwa mijibu wa sera na sheria  mbalimbali zinazohusu ardhi zimeweka wazi umuhimu wa kuwepo mpango wa matumizi bora ya ardhi kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa hadi taifa, hivyo yeye akiwa ni mbobevu kwenye eneo hilo anaamini ndio njia inaweza kupunguza au kumaliza migongano ya binadamu na wanyamapori nchini.          

“Unajua ukipitia Sera ya Ardhi ya mwaka 1995, Sera ya Uhifadhi Wanyamapori 2009, Sera ya Misitu na Mazingira, Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999, Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na nyingine zinasisitiza umuhimu wa kuwepo mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa kila eneo ambao linahusu nchi yetu, hivyo tuwekeze huko,”amesema.     

Mtafiti huyo amesema hata Mpango wa Taifa wa Matumizi Bora ya Ardhi wa mwaka 2013 hadi 2033  unaelekeza kuwepo kwa mpango huo kwenye kila eneo kama njia muhimu ya kutatua changamoto za migongano ya binadamu na wanyamapori.                

Amesema mpango huo wa taifa unaelekeza wapi kunafaa kwa matumizi ya hifadhi, makazi, kilimo, misitu na mengine.

Mtafiti huyo amesema pia mpango unahusisha kanda, mikoa, wilaya na vijiji na kwamba juhudi zimeanza kuonekana kwa baadhi ya kanda na wilaya kutekeleza.                

Dk Nindi amesema migongano ya binadamu na wanyamapori ambayo inatokea kwenye shoroba na hifadhi zinasababishwa na kukosekana kwa mipango bora, hivyo ni wakati muafaka kutumia njia hiyo kuleta mabadiliko.                         

Mtafiti huyo amesema iwapo mpango wa matumizi bora ya ardhi utapewa msukumo ni wazi kuwa kila kundi litatekeleza kazi zake kwa uhuru na amani bila kuingia kwenye migongano.                           

“Faida ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ni kusaidia wakulima, wafugaji, makazi na shughuli nyingine kufanyika katika maeneo yake bila kuingiliana, kinyume na hapo kila siku tutakuwa tunashuhudia migongano,” amesema.

Dk Nindi amesema kubwa zaidi linaweza kutokea kupitia uwepo wa mpango huo ni kukuza uchumi wa nchi na wananchi.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Dk Fortunata Msofe amesema  katika kukabiliana na migongano baina ya binadamu na wanyamapori wizara imeandaa mkakati wa kitaifa mwaka 2020 na kwa sasa wanatekeleza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika maeneo yote ya nchi hasa hifadhi.                        

Amesema migongano baina ya makundi hayo ipo katika nchi zote za Afrika ikiwemo Tanzania, ila kwa kushirikiana na GIZ wanaendelea kuutekeleza katika maeneo mbalimbali ikiwamo Tunduru, Namtumbo mkoani Ruvuma na Liwale mkoani Lindi.                        

“Tanzania ina takribani theluthi moja ya ardhi ambayo imehifadhiwa ambapo kuna hifadhi za taifa 21, mapori ya akiba 29, mapori tengefu 23 na Maeneo ya Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori (WMA) 38 na 24 yamepata hati ya matumizi na kusaidia jamii kushiriki kwenye uhifadhi na kupata kipato, yote hayo yanaweza kuwa endelevu kupitia mkakati huo wa serikali,” amesema.             

Amesema mpango mkakati huo ulianza mwaka 2020 unafikia ukomo mwaka huu na matarajio yao kwa kushirikiana na wadau wengine kama GIZ watauhuisha.                          

Dk Msofe amesema mpango mkakati umegusia maeneo ambayo yana changamoto nyingi hasa kwa kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi, pamoja na wananchi kuweza kutoa taarifa kwa haraka pale ambapo migongano ya binadamu na wanyamapori inavyotokea ili kuepusha madhara.                              

Moja ya eneo ambalo wamelipa kipaumbele ni Ukanda wa Ruvuma ambao unahusisha wilaya hizo tatu na vijiji 30 ambavyo vina changamoto kubwa.       

Amesema pia wamekuwa wakitoa elimu kwa maofisa wanyamapori na wengine ambao wanahusika na sekta hiyo.                                       

Mkurugenzi huyo amesema pia wana mfumo wa kutatua mgongano wa wanyamapori ambao kwa sasa wanapambana kuhakikisha kuwa wanausambaza kwenye wilaya zote zenye migongano.                           

Amesema kupitia mradi wamehakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi ambazo zitawezesha sekta hiyo inakuwa na faida zaidi kwa jamii.

 “Serikali itaendelea kushirikiana na GIZ kuhakikisha changamoto zinazotokea kwenye maeneo ambayo ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori inapungua,” amesema.

Aidha, Dk Msofe amewashauri wananchi wanaokabiliana na migongano baina ya binadamu na wanyamapori wajikite kwenye kilimo cha pilipili ambacho sio rafiki kwa tembo ambao ni moja ya wanyama wanaosababisha migongano.                          

Mkurugenzi huyo amesema mradi huo utawezesha vijiji na wilaya husika kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi, hali ambayo itachochea ukuaji wa uchumi kwa haraka.                                   

Naye Ofisa Wanyamapori kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Mwichage amesema GIZ imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi hasa katika eneo la uhifadhi na kuweka wazi TAMISEMI itaendelea kuipa ushirikiano kwani jamii inayoguswa ipo chini yao.                             

Amesema Mradi wa Kutatua Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori unapaswa kuendelezwa kwani unasaidia jamii hasa ya Ukanda wa Ruvuma.            Amesema migongano baina ya binadamu na wanyamapori imekuwa ikiongezeka kutokana na kasi ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yapo duniani kote.                       

Amesema Mkoa wa Ruvuma umeanzisha WMA 30 ambazo zinanufaika na biashara ya carbon, huku zikichochea utunzaji wa mazingira.                            

Ofisa huyo amesema ili kampeni hiyo ya kutatua migongano baina ya binadamu na wanyamapori waandishi wa habari wanapaswa kuongeza kasi kutumia kalamu zao, ili jamii iweze kuelewa na kuchukua hatua sahihi kwa maslahi yao na nchi.   

“GIZ ni wadau muhimu katika mipango na mikakati ya serikali kumaliza migongano baina ya binadamu na wanyamapori naamini, kila mdau akishiriki kwenye upande wake hili litawezekana. Nawaomba ndugu zangu waandishi wekeni mkazo kwani nyie mnaweza kuwafikia watu wengi na kwa lugha rahisi,” amesema.                             

Mkurugenzi Mkuu wa JET, John Chikomo amesema chama hicho kimeweka mkazo wa mafunzo kwa waandishi wa habari ili kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi kuhusu mradi huo ambao unatekelezwa na GIZ.                                        

“Sisi JET tumetengeneza kundi la waandishi wa habari za mazingira ambao watatumia muda wao kuelezea mradi huu na mingine ambayo ina lengo la kulinda shoroba na hifadhi zetu, ili kila muhusika aweze kufahamu na kufanyia kazi,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Mpina amng’ang’ania Bashe, kumburuza mahakamani pamoja na bodi ya sukari

Spread the loveMbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) amesema amenuia kumpeleka mahakamani...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Majahazi yadakwa na madumu 1,731 ya mafuta ya kupikia

Spread the loveKikosi kazi cha Polisi Wanamaji Dar es Salaam kimekamata majahazi...

Habari Mchanganyiko

Watuhumiwa wa mauaji ya mtoto mwenye ualbino wafikishwa mahakamani

Spread the loveWATUHUMIWA wa mauaji ya Asimwe Novath, mtoto mwenye ualbino, wamefikishwa...

Habari Mchanganyiko

Sangoma awaponza vijeba, watupwa jela maisha kwa kubaka wanafunzi

Spread the loveMAHAKAMA ya wilaya Nkasi Mkoani Rukwa, imemhukumu kifungo cha maisha...

error: Content is protected !!