Tuesday , 19 March 2024
Home Kuhusu sisi

Kuhusu sisi

SERA YA JUMLA YA MwanaHALISI Online

Kwa kuwa nchi yetu – Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – inafuata mfumo wa utawala wa kidemokrasia unaotambua kuwepo vyama vingi vya siasa – kama inavyoelekezwa katika sehemu ya UTANGULIZI ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 – basi gazeti letu la Mtandaoni la MwanaHALISI Online litakuwa linalochapisha habari na makala zinazoielekeza jamii kufikia Taifa lenye neema kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni, chini ya demokrasia ya kweli.

Na kwa kuwa “demokrasia ya kweli” inatafsiriwa kama mfumo unaowezesha wananchi kuamua mambo yao kupitia utaratibu wa Katiba (ambayo ndiyo mkataba wao kitaifa wa kuongozwa) unaochagizwa na uongozi unaojali na kuheshimu Sheria, Kanuni na Taratibu, uandishi wa habari wa gazeti la MwanaHALISI Online siku zote utakuwa unaoshikilia mtizamo huo.

Ili kutekeleza jukumu la kikatiba la kujenga jamii yenye uelewa wa wajibu wake kwa taifa, gazeti litakuwa la kuangaza, kuchambua, kushauri na kupeleka ujumbe kwa umma. Tunatambua kwamba umma na wasomaji wetu hususan, wanastahili habari, makala na taarifa zilizoshiba maelezo na ambazo ni za kweli na kweli tupu; zilizo sahihi na ambazo zimeandikwa kwa utaratibu mzuri unaojali maadilli ya kitaaluma. Uwasilishaji wa habari na makala zetu, wenyewe unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuvutia wasomaji.

Gazeti la MwanaHALISI Online litakuwa linalojielekeza katika kuwapa wananchi – iwe mtu mmoja mmoja, kikundi au jamii iliyopo kwa mujibu wa sheria za nchi – fursa ya kutoa maoni kuhusu jambo lolote lile linalohusiana na namna serikali yao inavyoendeshwa. Tunatambua ukweli kwamba kwa kuwa mamlaka ya nchi ni wananchi wenyewe, kama inavyotajwa na Katiba, basi ni vema wakapewa nafasi ya kushiriki shughuli za kuendesha nchi yao.

Katika jukumu hilo, vyombo vya habari, kama sehemu muhimu katika jamii, likiwemo gazeti la MwanaHALISI Online, vinao wajibu wa kikatiba wa kuinua sauti za wananchi ili kutekeleza lile fungu liitwalo WAJIBU WA JAMII – katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalojumuisha Ibara 24-30 za katiba hiyo.

Gazeti litakuwa linasaidia na kurahisisha ushiriki wa wananchi katika uendeshaji wa mambo yanayohusu jitihada zao katika kuyafikia maendeleo yao binafsi kupitia shughuli za uzalishaji mali kwa namna yoyote ile; pamoja na wajibu wao katika kuchangia ujenzi wa uchumi wa taifa.

Kisera, tunaposema Serikali, tunalenga kutambua kuwepo kwa mihimili mitatu (Pillars of Nation) inayotajwa na Katiba katika dhana ya mgawanyo wa madaraka – Serikali (Utawala), Bunge (Chombo cha kutunga sheria na kuisimamia serikali katika utekelezaji wake wa kila siku wa majukumu ya kikatiba), na Mahakama (Chombo cha kutafsiri sheria).

Kwamba habari, makala pamoja na picha na michoro itakayoendana nazo kuchapishwa gazetini zitahakikishwa kuwa zinazofuatana na mtizamo huo; huku nyenzo kuu za kitaaluma zikizingatiwa kwa ukamilifu wake. Nyenzo hizi ni UKWELI, USAHIHI, UWAZI, UWIANO, kujali HISHIMA ya faragha na ubinaadamu hata kama ipo sababu ya msingi ya mtu fulani kuhusishwa na habari husika.

Tuna maana kwamba uongozi wa gazeti wakati wote katika utendajikazi wake utakuwa unaongozwa tu na yanayoendana na maamuru ya Katiba na Sheria za nchi, pamoja na mikataba ya kimataifa inayohimiza HAKI YA KUJUA na HAKI YA KUJIELEZA. Haki ya kulinda vyanzo vya taarifa mbalimbali na kutunza nyaraka zitakazotumika kujenga habari na makala zetu, itakuwa ni jambo la kusimamiwa vilivyo na uongozi wa gazeti.

Tunaahidi kuwa makini zaidi katika eneo hili kwa sababu tunayo hakika linachangia kwa kiwango kikubwa kujenga heshima ya gazeti na watendaji wake pale chanzo cha taarifa kinapoamini kuwa kitakuwa huru pasipo shaka yoyote iwapo hakitotajwa kwa namna yoyote ile katika habari husika na baada ya kuchapishwa.

Tunaamini kuwa tunu hizi mbili za msingi wa kibinadamu, hazistahili kuwekewa mipaka ili kuzikwaza, almuradi tu kuzingatiwa kwake kiutendaji kunafuatana na msingi wa Katiba ambayo ndiyo sheria mama katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni sera ya gazeti la MwanaHALISI Online kuwa katika utendaji wake wa kila siku, halitakuwa linalotenda kazi kwa nia ya kumuonea mtu au kundi lolote katika jamii; hakutakuwa na mwenendo wa kutoa habari au makala inayolenga kwa makusudi kumchafua mtu au kundi lolote katika jamii zaidi tu ya kuwa habari au makala itakuwa imezingatia ukweli kwamba katika kuchapishwa kwake, ina umuhimu unaostahili kwa kulingana na maslahi halisi ya umma.

Na kwamba kazi ya uandishi wa habari chini ya MwanaHALISI Online itatekelezwa kwa weledi na uadilifu wa kiwango cha juu, kulingana na msingi wa maadili unaotakiwa kitaaluma badala ya kufikiria kutenda kwa woga, upendeleo au chuki ya namna yoyote ile. Daima uongozi wa gazeti utakuwa wazi na wenye moyo mweupe kwa mtu yeyote awaye, kundi au taasisi yoyote katika jamii na zaidi ya hapo, anayehisi hakutendewa haki katika moja ya habari au makala iliyochapishwa gazetini. Hii itasimamiwa kwa mujibu wa taratibu za kitaaluma za kutoa nafasi ya haki kwa mhusika, ya kusikilizwa.

Kutokana na Sera ya Jumla, gazeti la MwanaHALISI Online linaahidi kusimamia jukumu lake la kikatiba la kupasha habari mbalimbali kwa minajili ya kusaidia umma na taifa kufikia maendeleo yanayozingatia nyanja/sekta zote za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni. Utekelezaji utazingatia tija katika sekta tajwa kulingana na matakwa ya umma wenyewe na kwa namna ambavyo serikali inatekeleza jukumu lake la kikatiba la kuhudumia wananchi.

Katika mwelekeo huo, ni ahadi ya uongozi kwamba Gazeti la MwanaHALISI Online kupitia habari na makala zake, litakuwa linatoa mchango wake katika kuisaidia Serikali kutekeleza majukumu yake. Utekelezaji unaozingatia misingi ya kidemokrasia – inayoelekeza viongozi kuhiyari utamaduni wa uongozi bora, utawala bora na utawala wa sheria. Mambo haya yanahitaji kutiliwa mkazo kwa kuwa yanajenga msingi huo wa kuiwezesha serikali kuwa inayowajibika kwa watu wake, watu ambao ndio waliotoa mamlaka kwayo kuongoza.

Gazeti la MwanaHALISI Online litakuwa mbele kuhakikisha wananchi wanafaidi kikamilifu tunu ya uhuru wa kueleza fikira zao kuhusu serikali yao na viongozi wao kwani, kwa njia hiyo, watakuwa wanatimiza wajibu wao wa kikatiba.

Tunaahidi kuchapisha habari zilizofanyiwa utafiti wa upeo kupitia waandishi tulionao katika kitengo cha Uandishi wa Habari za Kiuchunguzi – Investigative Journalism Unit (IJU). Nia ni kuwa na habari na makala zenye tija zitakazolenga kuhimiza – kwa njia ya maoni, uelekezaji na ushauri – ujenzi endelevu wa miundombinu mbalimbali inayojulikana kuwa ndio njia mjarabu ya kufanikisha jukumu la serikali katika kukuza uchumi wa nchi.

Ujenzi huo utatarajiwa kuwa unaoendana na matumizi mazuri/bora ya ardhi pamoja na maliasili nyinginezo ambazo nchi imejaaliwa kuwa nazo: Mbuga za wanyama na hifadhi za taifa; mapori ya akiba, misitu, mito, maziwa, milima, madini na kadhalika.

Ni imani yetu kubwa kwamba maendeleo makubwa yatafikiwa katika nchi iwapo maliasili hizi zitatumika ipasavyo. Gazeti likiwa ni wakilishi wa sauti ya wananchi, litakuwa na utendaji unaohakikisha kutoa mchango wake wa kusaidia lengo hilo kufikiwa. Tutachapisha habari na makala zinazoshajiisha uongozi kuamini katika matumaini ya wananchi kimaendeleo; ari ya kujali utu na heshima ya Mtanzania; desturi, mila, silka na tamaduni za Watanzania zinazokubalika.

Tuwasiliane

MwanaHALISI Online (MHO),

Hali Halisi Publishers Limited (HHPL),

Kasaba Street,

Plot 57/31A Kinondoni,

P.O. Box 61747

Dar es Salaam.

TANZANIA.

Email: info@mwanahalisionline.com

Websites:     http://mwanahalisionline.com/

                     http://www.mwanahalisi.co.tz/

                     http://mwanahalisiforum.com/forum

Kama unamalalamiko kuhusu MwanaHALISI Online tuandikie kwa email  info@mwanahalisionline.com

Fika Ofisini kwetu kwa mawasiliano zaidi

error: Content is protected !!