KUPANDA kwa bei ya mafuta nchini kumeendelea kuwa mwiba mkali kwa wananchi wa kipato cha chini, huku athari zake zikienea kwa kasi katika sekta mbalimbali za maisha ya kila siku. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Wakati mamlaka zikitoa maelezo ya mabadiliko ya bei kulingana na soko la dunia, uhalisia unaowakumba wananchi wa kawaida ni tofauti kabisa ni maisha yanayozidi kuwa magumu kila kukicha.
Sekta ya usafirishaji ndiyo imekuwa mhanga mkuu wa ongezeko hili. Madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda, ambao kwa kiasi kikubwa hutegemewa na wananchi wengi kwa usafiri wa haraka na nafuu, wamelazimika kupandisha nauli ili kukabiliana na gharama za mafuta.
Safari iliyokuwa ikigharimu Sh. 1,000 sasa imefikia Sh. 2,000, mfano kutoka Tandale Uzuri hadi Manzese ilikuwa 1,000 baada ya jana kupanda kwa mafuta safari hiyo imekuwa ni 2,000 huku iliyokuwa Sh. 2,000 kutoka Sinza hadi Kinondoni Vijana imepanda hadi kuwa 3,000. Ongezeko kubwa ambalo linaathiri moja kwa moja mifuko ya wananchi wa hali ya chini.
Aidha, huduma za usafiri mtandaoni kama Bolt nazo zimeathirika kwa kiasi kikubwa, bei zimeongezeka na kufanya huduma hizi ambazo hapo awali zilionekana nafuu kwa baadhi ya watu, sasa kuwa anasa kwa wengi.
Kwa mtu anayehitaji usafiri wa kila siku kwenda kazini au kufanya shughuli ndogondogo za kujipatia kipato, hali hii imekuwa kikwazo kikubwa.
Changamoto hii haishii kwenye usafiri pekee, kupanda kwa gharama za usafirishaji kunasababisha pia kupanda kwa bei za bidhaa sokoni.
Wafanyabiashara ulazimika kuongeza bei ili kufidia gharama za usafirishaji na mwisho wa siku, mlaji wa mwisho ndiye anayebeba mzigo wote.
Hapa ndipo wananchi wa kipato cha chini wanapoathirika zaidi, kwani kipato chao hakiongezeki sambamba na gharama za maisha.
Swali la msingi linalobaki, hali hii itaendelea hadi lini? Je, kuna hatua madhubuti zinazochukuliwa kulinda maslahi ya wananchi wa kawaida? Wakati majibu yakisubiriwa, ukweli unabaki kuwa kila ongezeko la bei ya mafuta lina maana ya kupungua kwa uwezo wa mwananchi wa kawaida kumudu maisha.
Ni wakati sasa kwa wadau wote Serikali, sekta binafsi na wadhibiti wa nishati kukaa pamoja na kutafuta suluhisho la kudumu.
Bila hatua za makusudi, pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho litaendelea kupanuka, huku mzigo ukibaki kwa wale ambao tayari wanahangaika kila siku kutafuta riziki.
Kwa sasa, kilio cha wananchi kinasikika wazi: maisha yamekuwa magumu, na wanahitaji suluhisho sio maelezo tu.
Wakati hayo yakiendelea Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imewataka wadau wote wa sekta ya usafirishaji nchini, kutopandisha nauli kwa kigezo cha kupanda kwa bei za mafuta na badala yake wafuate utaratibu rasmi utakaowekwa na watakaopandisha hawatasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Akitoa kauli hiyo Kibaha mkoani Pwani wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mkuu wa Latra CPA. Dk. Habibu Suluo, amesema tarehe 8 Aprili 2026 ndio kitafanyika kikao cha wadau kujadili jambo hilo jijini Dar es Salaam.
Akaongeza kuwa wasafirishaji wanapaswa kujua kuwa hata wananchi bei hizo mpya zinawaumiza na hivyo nao wawe na huruma nao siyo kukimbilia tu kupandisha bei ya nauli.
Mkurugenzi huyo akaongeza kuwa wasafirishaji wote wanaotaka nauli zipande waje na maelezo ya kina namna wanavyotaka ipande na iwe kwa kiasi gani kwa mujibu wa sheria zinavyowataka.
Asichokijua Mkurugenzi huyu ni kwamba bei tayari imeshapanda kila kona hususani wasafirishaji wa vyombo vya moto wa pikipiki na bajaji.
Suala la mafuta ni suala ambalo limeleta mjadala mpana bungeni,Wabunge mbalimbali wakitoa maoni yao kuhusu changamoto hiyo,
ZINAZOFANANA
Je, Unajua unaweza kurejesha pesa yako mara 100% na Meridianbet?
Mahakama Bunda yamuachia Katibu Bavicha, wenzake 13
Watu 518 waliuawa 29 Oktoba