TUME ya Rais ya Uchunguzi wa matukio ya 29 Oktoba mwaka jana, imedai kuwa takribani watu 518, waliuawa kwenye maandamano ya kupinga uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea). Akiwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassa, Ikulu jijini Dar es Salaam, leo tarehe 23 Aprili 2026, mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mohammed Chande Othman, alieleza kuwa vifo hivyo, vilitokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba mwaka jana. Amesema, vifo vingi vimetoka na watu kupigwa risasi; miili 485 kati ya 518 ilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu kutoka vituo vya afya kwa ajili ya mazishi. Alisema, maiti sita hazikutambuliwa na hivyo, kuzikwa kwa mujibu wa kanuni ya utupaji wa taka na miili ya binadamu ya mamlaka ya serikali za mitaa. Alisema: “Kulifanyika uchunguzi wa maiti 260, maiti nyingine hazikufanyiwa uchunguzi kutokana na kukoseka kwa ridhaa ya ndugu zao kwa haraka ili wakazike. “Vifo 197 sawa na asilimia 90 na vifo 22 sawa na asilimia 10, havikuhusiana na matumizi ya silaha za moto. Kati ya maiti 260 zilizofanyiwa uchunguzi nyingi zilibainika zilikuwa na majeraha ya kutobolewa na vitu vya ncha kali na kuvunjika sehemu mbalimbali katika miwili.” Amesema, maiti 21 hazikuwa na majeraha, huku maiti sita zikiwa na majeraha ya moto. Alisema, bado kuna miili michache ambayo uchambuzi wa kinasaba haujafanyika, hivyo zinaendelea kuhifadhiliwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH). Hata hivyo, Jaji mkuu mstaafu Chande amesema, kauli yake kuhusu idadi ya vifo vilivyotokana na matukio hayo, siyo ya mwisho kwa kuwa upo uwezekano kuna watu wamekufa na kuzikwa na ndugu zao bila kupelekwa kwenye vituo vya afya. Alisema, “Kutokana na mazingira ya ghasia pamoja na madai ya baadhi ya mashahidi idadi ya vifo iliyobainiwa na Tume inaweza kubadilika kutokana na uwezekano wa kuwepo baadhi ya ndugu ambao walizika maiti ya wapendwa wao bila kuwafikisha kwenye vituo vya afya au hawakupata fursa ya kuja mbele ya tume.” Aidha, Jaji Chande amesema, upo uwezekano wa kuwepo kwa majeruhi ambao walitibiwa nje ya mifumo rasmi na kufariki taarifa zao kufikishwa panapostahili. Katika hatua nyingine, Jaji Chande ametoa wito wa kutaka kuwapo maridhiano ya kisiasa nchini na kupatikana Katiba mpya, kabla ya kumalizika mwaka 2028. Amesema, maridhiano hayo, yalenge katika kuliponya taifa na kuimarisha mshikamano wa kijamii, hasa katika masuala yanayohusu mabadiliko ya kisiasa na mchakato wa Katiba Mpya. Amesema, maridhiano hayo yasiishie kwenye suala la kisiasa, bali ni ajenda mtambuka inayohusisha sekta mbalimbali za jamii, zenye lengo la kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto za kisiasa zinazojitokeza nchini. Amefafanua kuwa mchakato wa Katiba Mpya unahitaji msingi imara wa mazungumzo, uvumilivu na uelewano wa kitaifa ili kuhakikisha kuwa maoni ya wananchi yanazingatiwa na hatimaye kupata katiba itakayokubalika na pande zote. Share this… Facebook Pinterest Twitter Linkedin Whatsapp About The Author Erasto Masalu See author's posts Post navigation Ripoti ya Tume yasubiriwa