Safari za ndege zaanza Iran baada ya kusitishwa kwa siku 57 za vita
BAADA ya kusitishwa kwa muda wa siku 57 kufuatia mapigano makali ya Mashariki ya Kati, safari za ndege zimeanza kurejea katika Imam Khomeini International Airport, ambao ni lango kuu la anga la mji mkuu wa Tehran.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Taarifa zilizotolewa zinaeleza kuwa anga ya Iran imefunguliwa tena, hatua iliyowezesha kurejea kwa safari za kimataifa, ingawa bado ni kwa kiwango kidogo ikilinganishwa na hali ya kawaida.
Kwa siku za kawaida, uwanja huo hupokea kati ya safari 100 hadi 150 za ndege kwa siku. Hata hivyo, kwa sasa idadi hiyo imeshuka kwa kiasi kikubwa hadi kufikia takribani safari 10 hadi 15 kwa siku, hali inayoonyesha kuwa shughuli za usafiri wa anga bado ziko katika hatua za mwanzo za kurejea katika hali ya kawaida.
Licha ya changamoto hizo, dalili za uhai zimeanza kuonekana, huku abiria wachache wakianza kujitokeza katika vituo vya uwanja huo, wakisubiri safari zao au kuwasili kutoka mataifa mbalimbali.
Ufunguzi huu unakuja wakati ambapo bado kuna athari kubwa za uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na vita katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Wataalamu wa usafiri wa anga wanakadiria kuwa inaweza kuchukua muda kabla ya shughuli kurejea katika kiwango cha kawaida, huku juhudi za ukarabati na kuhakikisha usalama wa anga zikiendelea kupewa kipaumbele.