WAKATI usafiri wa meli katika Mlango-Bahari wa Hormuz ukiwa umebanwa vikali kutokana na mvutano wa Iran na Marekani, meli ya kifahari ya Nord yacht inayohusishwa na bilionea wa Urusi Alexey Mordashov imefanikiwa kupita katika njia hiyo nyeti ya kimataifa na kutia nanga Muscat, Oman. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Takwimu za ufuatiliaji wa baharini zinaonyesha meli hiyo yenye urefu wa mita 142 na thamani ya zaidi ya dola milioni 500 iliondoka Dubai mwishoni mwa wiki na kuvuka Hormuz kuelekea Oman.
Kupita kwa meli hiyo kumewaacha wengi na maswali kuhusu namna ilivyopata ruhusa ya kutumia njia hiyo huku Iran ikiendelea kudhibiti kwa karibu usafiri wa meli katika eneo hilo, ambako kwa sasa ni meli chache sana zinazopita ukilinganisha na zaidi ya meli 100 zilizokuwa zikivuka kila siku kabla ya mzozo.
Mordashov anatajwa kuwa mmoja wa wafanyabiashara wa karibu wa Rais wa Urusi Vladimir Putin huku Urusi na Iran zikiendeleza ushirikiano wa kisiasa na kiusalama.
Mlango-Bahari wa Hormuz ni njia muhimu inayobeba karibu asilimia 20 ya mafuta ghafi na gesi asilia duniani, hivyo kuzorota kwa usafiri wake kumeendelea kusukuma bei ya mafuta kupanda, ambapo mafuta ghafi ya Brent yamefikia dola 109 kwa pipa.
Kupita kwa meli hiyo ya kifahari katikati ya vizuizi hivyo kumezua mjadala mpya kuhusu nguvu ya ushawishi wa matajiri wa Urusi ndani ya mgogoro unaotikisa uchumi wa dunia.