Rais Ruto kuhutubia Bunge la Tanzania Mei 5
RAIS William Ruto, Rais wa Kenya anatarajiwa kulihutubia Bunge la Tanzania tarehe 5 Mei 2026 kuanzia saa 5 asubuhi, katika tukio linalotarajiwa kuvutia hisia na mjadala mpana kuhusu mustakabali wa ushirikiano wa kikanda.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Tangazo hilo limetolewa bungeni leo Jumatano 29 Aprili 2026 na Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo ambaye ameomba wabunge kuhudhuria siku hiyo kwa wingi.
“Waheshimiwa wabunge, nawatangazia kuwa, siku ya Jumanne ya tarehe 5 Mei 2026, Rais Ruto, atalihutubia Bunge hili, katika hotuba hiyo ambayo itakuwa ya kitaifa pia,” amesema Sillo.
Sillo amesema mbali na Rais Ruto, viongozi wengine wa kitaifa pia watashiriki bungeni siku hiyo, hivyo akasisitiza ushiriki wa wabunge uwe wa kutosha siku hiyo ambayo alisema ni ya kihistoria.
Ujio wa Rais Ruto na kulihutubia Bunge umekuja ikiwa imepita miaka mitano tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipolihutubia Bunge la Kenya 5 Mei 2021.
Ziara ya Rais Ruto inatarajiwa kuwa fursa ya kujadili changamoto na fursa zilizopo katika ukanda huo, huku viongozi wa pande zote wakitarajia kuendeleza mshikamano na ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo jirani.