September 16, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Waziri Chana: Andaeni majina ya watoto kabla ya kuzaliwa

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Balozi Dk. Pindi Chana amewataka wazazi kujenga utaratibu wa kuandaa majina ya watoto wao mapema kabla ya kuzaliwa ili kwa haraka waweze kusajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa mara baada ya kuzaliwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Dk. Chana ametoa wito huo mwa wiki Jijini Dodoma wakati wa ziara yake ya kujionea zoezi la usajili linavyoendela sambamba na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika hospitali ya St. Gemma,Kkituo cha afya Makole na Zahanati ya Kikuyu zilizopo Jijini hapa.

“Leo nimetoa vyeti vya kuzaliwa kwa baadhi ya wakina mama waliojifungua salama na kuruhusiwa nyumbani,” alisema Dk. Chana.

“Nawaomba wazazi kujenga utaratibu wa kuandaa jina la mtoto mapema kabla ya kuzaliwa ili asajiliwe mara baada ya kuzaliwa na kupatiwa cheti kwani ni haki ya kila Mtanzania,” alisisitiza Dk. Chana.

Aidha, Balozi Chana amezitaka taasisi mbalimbali za umma na binafsi kuvipokea vyeti hivyo vinavyojazwa kwa mkono na kutolewa kwa wototo wa umri chini ya miaka mitano wanaosajiliwa katika Ofisi za Watendaji Kata na vituo vya Tiba kote nchini kwani ni vyeti halali na vina hadhi sawa na vyeti vinavyotolewa kwa njia ya compyuta.

“Nitoe rai kwa taasisi mbalimbali za umma na binafsi ambao huvipokea kwa ajili ya kuwapatia wananchi huduma,” alisema na kusisitiza umuhimu wa vyeti vya kuzaliwa kwa kila mtanzania.

Aidha, Dk. Chana amewataka wananchi kuchangamkia huduma hiyo inayotolewa bure nchi nzima, akisema kuwa vina mchango mkubwa katika kupata huduma mbalimbali, ikiwemo matibabu kupitia bima ya afya, elimu na baadaye ajira na kuzitaka taasisi mbalimbali za umma na binafsi kuvipokea vyeti hivyo kwa ajili ya kuwapatia wananchi huduma.

“Nipende kuipongeza RITA kwa kazi kubwa wanayoifanya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Watanzania wanapata vyeti vyao vya kuzaliwa na hili nimejiridhisha pasina shaka kazi hii kubwa ikiendelea kwa ufanisi mkubwa,” alisema.

Naye Dk. Flora Mwakalago ambaye ni Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya cha Makole, alisema wakati akielezea mafanikio ya kituo hicho toka kuanzishwa kwa huduma za usajili wa vizazi kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano mwaka 2019 kuwa zaidi ya watoto wachanga 550- 600 huzaliwa kila mwezi huku kati yao watoto 200- 250 wakipatiwa vyeti vya kuzaliwa.

“Kwa kipindi cha mwezi julai, 2023 hadi kufikia juni, 2024 tayari tumeshasajili na kuwapa vyeti vya kuzaliwa watoto zaidi ya 2,750 haya ni matokeo mazuri kwa kituo chetu,” alisema Dk. Mwakalago.

Naye, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kikuyu, Dk. Azania Silliah alisema kuwa kata ya Kikuyu Kaskazini ina jumla ya wakazi 14,654 ambapo wanawake ni 9,250 na kati yao wajawazito ni 705.

“Kuanzia mwezi Julai mwaka jana (2023) mpaka kufikia mwezi Juni (2024), tumesajili na kuwapatia vyeti watoto zaidi ya 642 sawa na asilimia 92%,” alieleza Dk. Silliah.

Mmoja wa wazazi waliopatiwa vyeti, Halima Abdallah, mbali ya kuishukuru serikali kwa kazi nzuri inayofanya ikiwemo uboreshaji na ujenzi wa vituo vya afya, alisema uwepo wa huduma hiyo inayotolewa bure nchi nzima umekuwa mkombozi, kwani kila mtoto anapata cheti cha kuzaliwa mara baada ya kuzaliwa na hivyo kuokoa gharama ambazo zingezitumia kukipata kwenye ofisi za RITA.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi alisema tangu zoezi hilo kusajili watoto wote chini ya miaka mitano watoto wengi wameweza kusajiliwa nchini nzima na mwamko umekuwa mkubwa.

“Naomba nikuhakikishie mheshimiwa Waziri kuwa RITA itahakikisha inamfikia kila mtoto anayepaswa kuandikishwa na kupata cheti cha kuzaliwa bure,” alisema Kanyusi na kuishukuru serikali ya Awamu ya Sita chini Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na wadau wote wa maendeleo kwa kuunga mkono zoezi hilo.

About The Author