December 13, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NFRA yaja na mfumo wa kidijitali kurahisisha ununuzi wa nafaka kwa wakulima

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umesema umejipanga kuimarisha vituo vya manunuzi ya nafaka nchini kwa kutumia mfumo mpya wa kidijitali ili kurahisisha manunuzi kutoka kwa wakulima na wafanyabiahsra wa nafaka hizo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma …(endelea).

Mfumo huu utasaidia taarifa za muuzaji wa nafaka kutumwa kwa haraka na kwa ufanisi kwenda mahali husika na kurahisisha mchakato wa malipo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Dk. Andrew Komba amesema mfumo huo mpya utaongeza ufanisi kwa kupeleka taarifa za muuzaji kwa meneja wa kanda na ofisi ya mkurugenzi mkuu kwa haraka kwa ajili ya utekelezaji na kuidhinisha malipo ili kuepuka urasimu unaoweza kujitokeza.

“Kimsingi, huu ndiyo mfumo mpya tunaoukusudia kuutumia katika kutoa huduma kwa haraka na ufanisi zaidi katika vituo vyetu vya manunuzi,” amesisitiza Dk. Komba.

Kwa sasa amesema kuwa NFRA ina vituo 72 vya manunuzi vilivyopo katika kanda nane hapa nchini.

Amezitaja kanda hizo kuwa ni Dodoma, Dar es Salaam (Kipawa), Njombe (Makambako), Songwe, Rukwa (Sumbawanga), Arusha (Babati), Shinyanga na Songea.

Katika vituo hivyo, Dk. Komba amesema wafanyabiashara wanapeleka mazao yao katika vituo hivyo kwa ajili ya mauzo.

Dk. Komba aliongeza kuwa ofisi yake ina mpango wa kuongeza idadi ya vituo hivyo, ili kuwasogezea huduma zaidi wakulima na wafanyabiashara.

Amesema lengo kwa sasa ni kuwa na vituo vipatavyo 100 nchi nzima na kuongeza idadi hiyo kadri inavyowezekana.

Amefafanua kuwa NFRA ina utaratibu wa aina tatu wa ununuzi, ukiwemo wa kununua nafaka kutoka kwa wakulima wadogo ambao huuza mahindi, mpunga, au mtama katika kanda zilizopo.

Amesema nafaka hizi hukaguliwa ili kukidhi ubora na muuzaji hulipwa ndani ya siku tano hadi 14 baada ya wahasibu kukamilisha taratibu zao.

Pili, amesema NFRA inanunua nafaka kuanzia tani 2000 na kuendelea kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa pamoja na kufanya manunuzi kutoka vyama vya ushirika ambapo wakulima hurasimisha mazao yao.

Kuhusu bei ya nafaka hizo, Dk. Komba amesema kuwa Serikali inawajali wakulima na mara kadhaa imekuwa ikitoa bei elekezi ili kuhakikisha wananufaika na shughuli zao za kilimo hapa nchini.

Dk. Komba amesema hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza bei elekezi ya Sh 700 kwa kilo moja ya mahindi na Sh 800 kwa kilo moja ya mpunga na NFRA inazingatia maelekezo haya katika kufanya malipo.

“NFRA inajitahidi kwa nguvu zote kuhakikisha kuwa mfumo huu mpya unaleta mabadiliko chanya katika ununuzi na usambazaji wa nafaka nchini,” amesema.

About The Author

error: Content is protected !!