NBC yazindua kampeni ya “NBC Shambani” Namtumbo
BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua rasmi kampeni yake ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde” katika mkoa wa Ruvuma, ikiwa na lengo la kuimarisha elimu ya fedha na kuchochea maendeleo ya kilimo biashara. Kampeni hiyo inalenga kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kimkakati—ikiwemo ufuta, soya, mbaazi na tumbaku—hususan katika wilaya za Songea, Namtumbo na Tunduru, kupitia utoaji wa huduma za kifedha zilizobuniwa mahususi kwa wakulima. Anaripoti Mwandishi Wetu, Namtumbo, Ruvuma … (endelea).
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika wilayani Namtumbo mwishoni mwa wiki ukiongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Francis Ngoroka, na kushirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, wakiwemo viongozi wa vyama vya ushirika pamoja na wakulima. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa NBC, akiwemo Meneja wa Kanda ya Pwani, Zubeider Haroun, na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo Wadogo na Wakulima, Raymond Urassa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ngoroka aliipongeza NBC kwa jitihada zake endelevu za kuwawezesha wakulima kupitia suluhisho bunifu za kifedha. Alibainisha kuwa ujio wa kampeni hiyo utachochea ukuaji wa uchumi wa wilaya ya Namtumbo na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla, hasa kupitia huduma jumuishi zinazojumuisha elimu ya fedha, huduma za bima, pamoja na mikopo ya maendeleo kwa wakulima na vyama vyao.

Alisisitiza kuwa thamani ya kipekee ya kampeni hiyo inaonekana katika msisitizo wake wa kujenga nidhamu ya fedha miongoni mwa wakulima na vyama vya ushirika. Hatua hiyo, alisema, itawawezesha wakulima kuelewa umuhimu wa kuweka akiba, kutumia huduma za bima—ikiwemo bima ya afya na mazao—na kuwekeza katika zana za kisasa za kilimo ili kuongeza tija na kupunguza hatari.
“Mpango huu utahamasisha wakulima kujiunga na mifumo rasmi ya kifedha, hatua itakayochochea uchumi jumuishi na kuongeza ustahimilivu wa sekta ya kilimo,” alieleza, huku akiwahimiza wakulima kutumia fursa hiyo kwa kufungua akaunti za NBC Shambani.
Akifafanua zaidi, Urassa alisema kampeni hiyo itatekelezwa kwa kipindi cha miezi minne kuanzia mwanzo wa mwezi Juni hadi mwisho wa mwezi Septemba, ikihusisha utoaji wa mafunzo ya kina kuhusu huduma za kifedha zinazolenga sekta ya kilimo. Huduma hizo ni pamoja na bima ya mazao na afya, huduma za uwakala wa benki, suluhisho za kidijitali, pamoja na mikopo ya pembejeo na zana za kilimo.
Aidha, kampeni hiyo itaambatana na motisha mbalimbali kwa washiriki watakaofanya vizuri, zikiwemo zawadi za simu janja, pikipiki na kompyuta mpakato (laptop) kwa wakulima binafsi, vyama vya msingi (AMCOS) na vyama vikuu vya ushirika. Ili kushiriki, wakulima wanahitajika kufungua akaunti ya NBC Shambani na kupitisha miamala yao kupitia akaunti hizo.

“Lengo kuu ni kuwahamasisha wakulima kuhifadhi fedha zao katika mifumo rasmi ya kifedha badala ya njia zisizo rasmi. Kupitia kampeni hii, tunatoa akaunti zisizo na makato ya kila mwezi, mikopo ya zana za kilimo kama matrekta kwa wakulima mmoja mmoja, pamoja na mikopo kwa vyama vya ushirika kwa ajili ya pembejeo na mahitaji mengine muhimu ya uzalishaji,” alifafanua Urassa.
Aliongeza kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya mchango wa NBC katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kufanikisha ajenda ya kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo kutoka asilimia 5 hadi 10 ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wao, wawakilishi wa wakulima wilayani humo, Ismail Said wa Twendepamoja AMCOS na Shida Ntine wa Mliwasi AMCOS, walieleza kuridhishwa kwao na huduma zinazotolewa kupitia kampeni hiyo. Walisisitiza kuvutiwa na akaunti ya NBC Shambani isiyo na makato ya kila mwezi, pamoja na mafunzo ya elimu ya fedha na huduma za bima.
“Huduma za bima ya afya na mazao ni muhimu sana kwetu sisi wakulima, hasa katika kukabiliana na changamoto zisizotarajiwa. Pia elimu ya fedha itatusaidia kupanga na kusimamia mapato yetu kwa ufanisi zaidi,” alieleza Ntine, akisisitiza umuhimu wa kampeni hiyo katika kuboresha ustawi wa wakulima na familia zao.