PUNCLINE Africa imetangaza rasmi uzinduzi wa Punchline International Comedy Festival (PICF) 2026, tamasha la kimataifa la vichekesho litakalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 25 Mei hadi 1 Juni 2026. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea). Tamasha hili litawakutanisha wachekeshaji kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa kipindi cha wiki moja, likijumuisha maonesho mbalimbali, shughuli za vyombo vya habari, pamoja na ubadilishanaji wa utamaduni. Tamasha litafikia kilele chake kwa Grand Finale kubwa itakayofanyika Superdome. PICF 2026 itajumuisha maonesho ya vichekesho ya lugha ya Kiingereza na Kiswahili, ikiwa ni sehemu ya kuonesha utofauti na utajiri wa vipaji vya vichekesho barani Afrika. Mbali na burudani, tamasha hili linaweka mkazo katika umuhimu wa vichekesho kama sehemu ya ustawi wa afya ya akili (mental wellness), kwa kuwapa watu nafasi ya kucheka, kutafakari, na kupumzika kutoka changamoto za maisha ya kila siku. Katika kipindi ambacho watu wengi wanapitia changamoto binafsi na za kijamii, PICF inalenga kuonesha kuwa kicheko ni njia muhimu ya kujenga faraja, kuleta watu pamoja, na kuboresha hali ya kihisia. Akizungumza kuhusu tamasha hilo, Mwanzilishi Mwenza wa Punchline Africa, Evans Bukuku, alisema: “Comedy siyo kuchekesha tu. Ni njia ambayo watu wanatumia kuelewa maisha, kupunguza msongo wa mawazo, na kuunganishwa. Kupitia PICF, tunataka kuunda nafasi ambayo watu wanaweza kukutana, kucheka, na kuondoka wakiwa na nafuu zaidi, hata kama bado tunakabiliana na changamoto za maisha ya kila siku.” Kwa upande wake, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie Ave, alisema wameamua kuunga mkono tamasha hili kwa sababu wanaamini katika nguvu ya sanaa ya uchekeshaji, hasa kwa vijana wa Tanzania wenye vipaji vikubwa na ubunifu wa hali ya juu. “Vijana wengi wana vipaji na wanazalisha maudhui yenye ubunifu mkubwa, lakini mara nyingi hawajitokezi kutokana na aibu. Tunaamini jukwaa hili litawasaidia kujiamini zaidi, kujitokeza, na hata kuwafungua milango ya kufikia ngazi ya kimataifa,” alisema. Alieleza kuwa Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa tamasha hili kutokana na nafasi yake kama kitovu cha Afrika Mashariki, pamoja na historia yake katika harakati za Pan-Afrika. “Tukirejea historia, Tanzania ni sehemu muhimu ambako harakati za umoja wa Afrika zilianzia. Tunaamini kupitia vichekesho, Tanzania inaweza kuendelea kuunganisha Afrika kwa njia ya kipekee zaidi ya ucheshi na ucheshi wima,” aliongeza. Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Filamu Tanzania, Emmanuel Ndumukwa, alisema wanafurahia kuona tasnia ya uchekeshaji ikiendelea kukua kwa kasi nchini, na kupongeza juhudi za Punchline Africa kwa kuandaa tamasha hilo. “Hii ni hatua kubwa na inaweza kuwa mwanzo mpya (breakthrough) kwa tasnia ya ucheshi Tanzania. Serikali ipo tayari kuunga mkono juhudi kama hizi kupitia mifuko ya utamaduni, na tunasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa vigezo vya wazi ili kutoa fursa sawa kwa wote wenye sifa ya kushiriki,” alisema. Kwa upande wake, mwakilishi wa wacheshi wa Tanzania, Humphrey Richard maarufu kama MC Kisoli, alisema ana matarajio makubwa juu ya tamasha hilo, akisisitiza kuwa lina uwezo wa kubadilisha maisha ya wacheshi wengi. “Tamasha hili lina lengo la kweli la kuinua maisha ya wacheshi nchini na barani Afrika kwa ujumla. Zaidi ya burudani, ni jukwaa la kujifunza, kubadilishana utamaduni, sanaa na uzoefu. Hili si tamasha la kundi fulani la watu, bali ni la kila mtu, na kila mmoja anakaribishwa kushiriki,” alisema. Aliongeza kuwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, ikiwemo Ubalozi wa Ufaransa, umekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha tamasha hilo. Tamasha hili linalenga kuinua hadhi ya comedy kama chombo muhimu cha kitamaduni, si kwa burudani tu, bali pia kwa mazungumzo, uponyaji wa kihisia, na kutoa maoni kuhusu jamii, huku likiiweka Tanzania katika ramani ya matukio makubwa ya kimataifa ya vichekesho. Lakini pia, tamsha hili ni sehemu ya mradi wa Création Africa unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ufaransa na kuratibiwa na Alliance Française Dar es Salaam, unaolenga kuwawezesha wasanii na taasisi za ubunifu nchini. Kupitia mradi huu, Watanzania mbalimbali tayari wamenufaika kwa kupata rasilimali na fursa za kukuza vipaji na miradi yao ya ubunifu. Uzinduzi rasmi wa tamasha umefanyika kupitia mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumatano, tarehe 15 Aprili 2026, saa 4:00 asubuhi (10:00 AM), katika Punchline Comedy Club, Masaki, Dar es Salaam. Wawakilishi kutoka taasisi na wadau mbalimbali walikuwepo kushiriki na kutoa maoni kuhusu tamasha hilo. Tamasha hili linaandaliwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wakiwemo Ubalozi wa Ufaransa, Alliance Française, Tanzania Film Board, pamoja na SGA Security ambao watatoa huduma za usalama katika matukio yote ya tamasha. PICF inatarajiwa kuvutia hadhira kubwa kutoka makundi mbalimbali, ikiwemo vijana, wabunifu, pamoja na wadau wa burudani, huku ikiifikia hadhira ya zaidi ya watu milioni moja kupitia majukwaa ya kidigitali. Taarifa zaidi kuhusu wasanii watakaoshiriki, ratiba kamili ya matukio, pamoja na tiketi zitatolewa katika siku za hivi karibuni. Share this… Facebook Pinterest Twitter Linkedin Whatsapp About The Author Erasto Masalu See author's posts Post navigation EACOP yasaidia fedha vikundi 16 kuinua uchumi Tanga Hawa hapa wababe wanaowania kwenda Nusu Fainali Europa