February 27, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Kardinali Pengo aagwa kanisani kwake

 

MAMIA ya waumini wa Kanisa Katoliki nchini, jamaa pamoja na waombolezaji wengine, wamehudhuria misa ya kuuaga mwili wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Marehemu Kardinali Pengo aliyefariki dunia, tarehe 19 Februari 2026, atazikwa kesho Jumamosi, tarehe 28 Februari 2026, huko Pugu, jijini Dar es Salaam.

Pengo aliyefariki usiku wa Alhamis alipokuwa akipatiwa matibabu katika Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete. Alikuwa na umri wa takribani miaka 82.

Alifahamika kwa tabia ya upole na kuzungumza taratibu hata pale alipozungumzia masuala nyeti na mazito ya kiimani au kuikosoa mifumo ya uongozi wa kisiasa, serikali na viongozi wake.

Hata alipochokozwa alijibu kwa upole. Kuna wakati, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alimtolea maneno makali, lakini Pengo alipoulizwa na chombo kimoja cha habari, alijibu kuwa hamfahamu huyo askofu.

Tayari alikwishaeleza bayana anapendelea azikwe eneo la Pugu, lililopo takribani kilomita 25 nje ya jiji la Dar es Salaam na alijichimbia kaburi lake.

Polycarp Kardinali Pengo alizaliwa Agosti 5, 1944 huko Sumbawanga mkoani Rukwa.

Wakati wa uhai wake, Pengo alisema, eneo hilo alililependa na anatarajia uamuzi wake na chaguo lake hilo litaheshimiwa.

Alisomea Thiolojia ya Maadili mjini Roma katika Chuo Kikuu cha Pontifical Lateran, ambako alipata shahada ya uzamivu (udaktari) mwaka 1977.

Alifundisha Thiolojia ya Maadili katika Seminari kuu ya Kipalapala iliyo Tabora kwa muda mfupi, kisha akawa Gombera (Rector) wa kwanza wa Seminari Kuu ya Segerea jijini Dar es Salaam hadi mwaka 1983.

Aliteuliwa kuwa Askofu wa Nachingwea (sasa Lindi) mwaka 1983, na baadaye Askofu wa Tunduru–Masasi mwaka 1985.

Mwaka 1990 aliteuliwa kuwa Askofu Mwandamizi (Coadjuctor) Dar es Salaam, akingojea kustaafu rasmi kwa Laurean Kardinali Rugambwa. Mwaka 1992 akawa Askofu Mkuu wa Dar es Salaam kufuatia kustaafu kwa Kardinali Rugambwa ambaye alifariki dunia Desemba 1997.

Pengo alitangazwa kuwa Kardinali na Papa John Paul II katika mkutano wa makadinali (consistory) wa tarehe 21 Februari 1998.

About The Author

error: Content is protected !!