JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu sita kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Askari Polisi, Roland Mollel, yaliyotokea usiku wa 15 Aprili 2026 katika mtaa wa Mlimani, kata ya Muriet jijini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea). Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Justine Masejo, amesema mauaji hayo yalitokea kufuatia taharuki iliyozuka miongoni mwa wananchi baada ya kusambaa kwa taarifa kuwa kulikuwa na uwepo wa wezi katika eneo hilo. Amesema kuwa marehemu alikuwa ametoka kazini na alikuwa akiendelea na shughuli zake binafsi, ambapo alipita katika eneo hilo akiwa ameongozana na mtu mwingine anayedaiwa kuwa dereva wa bodaboda, wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki. Kwa mujibu wa kamanda huyo, kundi la wananchi waliokuwa na hasira lilianza kuwashambulia wawili hao kwa kuwatuhumu kuwa ni wezi, hali iliyosababisha kuwafukuza na hatimaye kusababisha kifo cha askari huyo. Kamanda Masejo ameongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa wengine waliohusika katika tukio hilo, huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini undani zaidi wa tukio hilo. Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuchukua sheria mkononi, likisisitiza kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa watu wasio na hatia. Share this… Facebook Pinterest Twitter Linkedin Whatsapp About The Author Fedrick Gama See author's posts Post navigation EACOP yasaidia fedha vikundi 16 kuinua uchumi Tanga