BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imeibuka mshindi kwenye Tuzo za Kimataifa za Ujenzi Zanzibar (ZICA Awards) baada ya kutunukiwa tuzo ya Benki Bora katika Kuwezesha Miradi ya Ujenzi Zanzibar (Excellence in Financing Construction Projects in Zanzibar), hatua inayothibitisha mchango wake mkubwa katika kukuza sekta ya ujenzi visiwani humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika mwishoni mwa wiki visiwani Zanzibar, ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chemba ya Taifa ya Biashara Zanzibar (ZNCC), Ali Suleiman Amour, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi kutoka serikalini na sekta binafsi. Benki ya NBC iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa na Uwekezaji, Elvis Ndunguru, aliyeongoza ujumbe wa maofisa wengine wa benki hiyo katika hafla hiyo.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Ndunguru alisema ushindi huo ni muendelezo wa mafanikio na uthibitisho wa jitihada endelevu za NBC katika kuwezesha miradi ya ujenzi nchini – Tanzania Bara na Zanzibar. Alitaja miongoni mwa miradi mikubwa iliyofanikishwa kwa ushiriki wa benki hiyo visiwani humo kuwa ni ujenzi wa Kituo cha Abiria cha Vivuko cha Maruhubi (Mpiga Duru) kilichozinduliwa hivi karibuni, pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kizimkazi.

“Kwa upande wa Tanzania Bara, NBC imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwezesha miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo miradi ya reli, madaraja na viwanja vya ndege. Tunatambua sekta ya ujenzi ni mhimili muhimu katika kukuza uchumi wa taifa, hivyo tutaendelea kushirikiana na serikali na sekta binafsi kuhakikisha miradi hiyo inafanikiwa, sambamba na kudhamini matukio muhimu ya wadau wa sekta hii,” alisema Ndunguru.
Benki ya NBC pia ilikuwa miongoni mwa wadhamini wakuu wa tuzo hizo za ZICA, ikionyesha dhamira yake ya dhati katika kuunga mkono maendeleo ya sekta ya ujenzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ZNCC, Ali Suleiman Amour, aliwapongeza waandaaji wa tuzo hizo — CSW Group na Zanzibar Marketing — pamoja na washindi wote, akizitaja tuzo za ZICA kama jukwaa muhimu la kuhamasisha ubora, ushindani wa kitaaluma na uwajibikaji katika sekta ya ujenzi.

Kutokana na mchango mkubwa wa sekta ya ujenzi katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia ukuaji wa miundombinu, biashara, utalii, makazi bora na uwekezaji, Amour aliziomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuimarisha ushirikiano zaidi, hususan katika kuweka sera na mazingira rafiki kwa wawekezaji wa sekta hiyo.
“Serikali pia ihakikishe inawajengea uwezo wazawa kupitia mafunzo, teknolojia na mitaji, sambamba na kusimamia viwango, ubora na ujenzi unaozingatia usalama na utunzaji wa mazingira. Kwa upande wa wadau wa sekta ya ujenzi, ni muhimu kuzingatia maadili, uwazi na sheria ili kujenga imani kwa jamii na serikali ambayo ndiyo mdau wao mkuu,” alisisitiza Amour.
Awali, akielezea mchakato wa utoaji wa tuzo hizo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa CSW Group, Annelise Nyangusi, aliwashukuru wadhamini wote wakiwemo Benki ya NBC, akibainisha kuwa vigezo vya kuwapata washindi vilijikita katika ubora wa huduma, ushirikiano wa soko pamoja na mbinu za kipekee za ufanisi wa kampuni.
ZINAZOFANANA
TAMISA: Wawekezaji sekta ya madini wapeni kipaumbele Watanzania
Jackpot ya bilioni 2 inaanzia na 500/= Tu kwa Meridianbet
Si bahati tu, ni uamuzi unaokupa ushindi kwenye Super Heli Premium