
MWENYEKITI wa UWT Taifa, Mary Pius Chatanda ameshuhudia utiaji saini wa mikataba mitano ya Sh. 13.3 bilioni zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja wilayani Rufiji. Anaripoti Joyce Ndeki, Pwani … (endelea).
Tukio hili la utiaji saini limefanyika Mei 7, 2025 mara baada ya kukamilika kwa ziara ya siku mbili ya Chatanda kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo, katika eneo la uwanja wa stendi wa Ikwiriri na kushuhudiwa na maelfu ya wananchi wa wilaya hiyo huku wasanii kadhaa wakitumbuiza kwa burudani za muziki.
Akitoa taarifa ya miradi hiyo, Meneja wa Wakala za Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Pwani, Leopold Runji amefafanua kuwa gharama hizo zinahusisha ukarabati wa barabara ya Nyamwage yenye Kilomita 28, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Chumbi- Kiegele yenye kilomita 1.4, ukarabati wa barabara ya Mohoro- Mtanga kilomita 12.3 na Mohoro Ndundutawa yenye kilomita 7.5.
Pia ukarabati wa barabara ya Nyamwage- Mpakani- Nambunju na ujenzi wa barabara za lami katikati ya mji wa Ikwiriri ambapo amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kuiunganisha wilaya hiyo na maeneo mbalimbali ya mikoa ya Tanzania.
Chatanda amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za miradi na kufafanua kwamba kwa kufanya hivyo siyo tu ametekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa mafanikio makubwa bali ameleta mapinduzi katika sekta ya miundombinu kote nchini.
Amempongeza Mchengerwa kwa kusimamia utekelezaji wa miradi yote kwa kiwango cha juu huku akitoa wito kwa maeneo mengine nchini kuiga utekelezaji huo.
”Ndugu zangu hapa ni vema tuwe wakweli, unaweza ukaletewa fedha za maendeleo lakini ukashindwa kutekeleza lakini,hivyo nampongeza mbunge wenu kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hii ambayo inakwenda kuleta tija kubwa kwa wananchi katika Wilaya ya Rufiji,” amefafanua Chatanda
Mbali na kukagua miradi ya Serikali pia ameshuhudia ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa chama, pia ameshuhudia mradi mkubwa wa ujenzi wa ukumbi wa kisasa wa wilaya unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.5 unaofadhiliwa na Mbunge wa Rufiji Mhe. Mchengerwa kwa kupitia marafiki na wadau mbalimbali.
Akizungumzia kuhusu miradi ya elimu katika wilaya hiyo, Chatanda amesema amefurahishwa na kazi nzuri ya ongezeko kubwa la Shule za Msingi na Sekondari na kutoa wito kwa wananchi kuwapeleka watoto wao katika shule hizo ili kuunga mkono maono ya Mhe. Rais ya kuwakomboa wananchi kielimu pia kwa manufaa makubwa ya taifa na vizazi vyao.
Mbunge wa Rufiji Mchengerwa amesisitiza kuwa Serikali imefanya kazi kubwa ya ujenzi wa shule ambapo amesema wakati anaingia kwenye ubunge kulikuwa na na Shule za Msingi 40 tu ambapo sasa kuna shule 63 na upande wa Vituo vya Afya, awali kulikuwa na vituo 3 na sasa vimefika 9, huku asimshukuru Mhe. Rais Samia kwa maono makubwa ya kuwaletea maendeleo watanzania.
Aidha, Chatanda alipotembelea na kukagua ukarabati wa hospitali ya Wilaya ya Rufiji na ujenzi wa kichomea taka katika eneo la Utete uliogharimu takribani Sh. 900 milioni na kuwataka wananchi kutumia huduma hizo ikiwa ni pamoja na wanaume kuwa msitari wa mbele kuwapeleka wake zao kwenye huduma za kliniki ili kujua afya za wenza wao na watoto.
Akizungungumzia kuhusu ukatili wa kijinsia, amewataka wazazi kuwalea watoto wao katika misingi maadili ili waweze kuja kuwa wazazi bora badala ya kuwaacha kujifunza kwenye mitandao.
ZINAZOFANANA
Kadinali Robert Prevost atangazwa kuwa Papa mpya
Bunge la Ulaya laitaka Tanzania kumuachia huru Lissu
NBC yaitambulisha “NBC Shambani’’ kwa wakulima wa Ufuta Pwani