Kazi ya tume ilikuwa kubaini hoja-Jaji Chande
MWENYEKITI wa Tume ya Uchunguzi wa ghasia zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi, Jaji Othman Chande, amesema jukumu kuu la tume hiyo lilikuwa ni kubaini ukweli kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa mbele yao.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Jumanne 28 Aprili 2026, Jaji Chande alieleza kuwa mchakato wa uchunguzi ulikuwa wa kitaalamu, ukilenga kuchambua hoja kwa msingi wa vielelezo na ushahidi wa moja kwa moja.
“Kazi ya msingi ya tume ilikuwa ni kubaini hoja, na kubaini huko ni fact finding kutokana na ushahidi uliowasilishwa mbele ya tume, pamoja na kujibu hadidu za rejea tulizopewa,” amesema Jaji Chande
Jaji Chande amefafanua kuwa hadidu hizo za rejea zilielekeza tume kuchunguza kwa kina mambo kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na kubaini chanzo cha ghasia hizo, malengo ya wahusika, pamoja na kuwabaini waliohusika moja kwa moja.
Aidha, amesema tume ilitakiwa pia kuchambua athari zilizotokana na matukio hayo, zikiwemo madhara ya kibinadamu, kiuchumi na kijamii, pamoja na kutoa mapendekezo ya namna ya kuzuia na kudhibiti matukio kama hayo yasijirudie siku zijazo.