WANAWAKE si washindani bali washirika wakuu wa wanaume katika kuiletea jamii maendeleo, hivyo kuna haja ya mchango wao kutambuliwa kwa kuwapa ushirikiano zaidi; badala ya kuwadharau na kuwakwamisha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea)..
Akihutubia mkutano wa uzinduzi wa mradi wa kukuza usawa wa kijinsia Tanzania kwa jina la PAMOJA, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia {WB}, Katibu wa BLM na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Injinia Zena Ahmed Said, anasema wanawake si watu dhaifu, ukweli unaothibitishwa na vitabu vitukufu ikielezwa kuwa kiwango chao cha ustahamilivu kinazidi cha wanaume.
Injinia Zena alisema mchango wa wanawake haujatambuliwa sawasawa, na kwa bahati mbaya, kwenye maeneo mengi, likiwemo la kuingia vyombo vya maamuzi, wanawake wanalazimika kuvuka vihunzi vingi kufikia malengo yao kutokana na mikwara ya wanaume dhidi yao.
“Sisi si washindani wa wanaume. Tuna wajibu wa kufanya kazi pamoja nanyi. Lazima wanaume mutambue mchango wetu wanawake. Inasikitisha wanaume wamejisahau wakatuacha wanawake katika kutambua utu wetu na haki yetu kwenye fursa za kimaendeleo,” alisema akilenga kuasa wanaume kukomesha kudhalilisha wanawake na watoto.
“Vipi mpaka leo mwanamke anawekwa pembezoni; tangu mtoto, anakaa jikoni huku mtoto wa kiume akisoma. Mwenyeezi Mungu katupa jukumu kubwa na muhimu sisi la kuzaa na kulea. Hatuko dhaifu maana hilo jukumu ni zito ambalo wanaume hawaliwezi. Basi ni haki yetu kutambuliwa kwa usawa zinapotokea fursa… zetu sote zisizojali jinsia,” alisema.

Akigusa tatizo kubwa la kudhalilisha na kukatili wanawake na watoto mbele ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Zanzibar, Anna Athanas Paul, Injinia Zena analalamikia kushamiri kwa utamaduni wa muhali unapokuja wajibu wa jamii kudhibiti uovu huo. Anasema “Pale mume anapomnyanyasa mkewe, atambue huyo ni mtoto wa watu. Ukiendelea hivyo, mbele unakuta mtoto wako wa kike anafanyiwa vile unavyomfanyia mamaake {mkeo}. Komesha dhulma hii. Usipochukua hatua hutafunga {goli}, sharti upige {mpira} ili ufunge.”
Injinia akatilia shime wanaume kujitokeza mbele kusaidia kufanikisha ushahidi kwenye matukio ya udhalilishwaji wanawake na watoto; na sio kuongoza kupindisha haki kwa kushauri maelewano. “Yule mtoto wa kike aliyedhalilishwa anafidiwa nini maishani mwake,” anashangaa na kuhoji mtindo huo unapingana na maamrisho ya Mwenyeezi Mungu asemapo kila mtu ni mchunga na {mbele ya safari} ataulizwa kwa alivyochunga.
Injinia anaasa wanaume kufikiria manunuzi wanayofanya kwa ajili ya familia zao kwa sababu yana mchango mkubwa katika makuzi ya mama na mtoto tangu mimba inapotunga. Lishe bora ni kitu muhimu, vinginevyo wanaume mnaongezea wanawake stress.
“Nyie wanaume msiendekeze mifumo ya kututia stress. Mkitupa stress mjue mnaharibu kizazi.”
Injinia ametambua jitihada za serikali zote mbili katika kumuendeleza mtoto wa kike na kuwapunguzia shida za kimaisha wanawake. Hatua mbalimbali zinazochukuliwa na viongozi wetu zinathibitisha ukweli huu,” anasema.
Mradi wa kukuza usawa wa jinsia kwa Zanzibar ambako wilaya nane zinahusika – Kaskazini A, B, Kati, Kusini Unguja; na Chake Chake, Mkoani, Wete na Micheweni kwa Pemba – unasimamiwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Zanzibar – Zanzibar Economic Empowerment Agency {ZEEA}. Ulianzia Tanzania Bara ambako kiasi cha Sh. 100 Bilioni kilitengwa kwenye utekelezaji.
ZINAZOFANANA
UNDP, Uingereza yawakutanisha viongozi wa vyuo vikuu kuchochea Ubunifu na Ujasiriamali Z’bar
TSL yazindua mpango wa ubunifu wa pamoja kupanua fursa za uwekezaji
Ayatollah Ali Khamenei: Kiongozi Mkuu wa Iran athibitika kuawa