February 24, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Lissu aibwaga Serikali, mahakama yakataa ushahidi nyongeza

 

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imekubali mapingamizi yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, dhidi ya notisi ya ushahidi wa ziada iliyowasilishwa na upande wa Jamhuri kupitia shahidi ACP Amini Mahamba katika kesi ya uhaini inayomkabili. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Katika uamuzi mdogo uliotolewa leo, Mahakama imeeleza kuwa notisi hiyo haikukidhi matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hivyo haiwezi kupokelewa kama sehemu ya ushahidi katika hatua ya sasa ya kesi.

Awali, tarehe 23 Februari 2026, Wakili Mkuu wa Serikali, Nassoro Katuga, aliieleza Mahakama kuwa upande wa Jamhuri uliwasilisha notisi hiyo ukiambatanisha ushahidi wa ziada wa ACP Mahamba, aliyekuwa kiongozi wa upelelezi wa matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025. Upande wa mashtaka ulidai kuwa waliutambua ushahidi huo wakati wa maandalizi ya shahidi huyo aliyepaswa kuanza kutoa ushahidi Februari 16, 2026.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Dunstan Ndunguru alisema Mahakama ilichambua hoja za pande zote mbili Jamhuri na utetezi ambazo zote zilijengwa kwa kutegemea kifungu cha 308 (1), (2), (3) na (4) cha sheria hiyo, kabla ya kufikia hitimisho kuwa notisi iliyowasilishwa haikukidhi vigezo vinavyotakiwa kisheria.

Jaji Ndunguru alifafanua kuwa kifungu hicho kinaruhusu kuwasilishwa kwa ushahidi wa shahidi ambaye maelezo yake yalikuwepo lakini hayakusomwa wakati wa mwenendo wa ukabidhi (committal proceedings), lakini hakitoi nafasi ya kuingiza ushahidi mpya ambao haukuwahi kuwepo au uliopatikana baada ya hatua hiyo kukamilika.

Mahakama pia ilibainisha kuwa kwa mujibu wa rekodi za kesi na maelezo ya upande wa Jamhuri, ACP Mahamba tayari alikuwa ametoa maelezo yake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati wa hatua ya ukabidhi. Hata hivyo, ushahidi wa ziada uliokusudiwa kuwasilishwa ulihusu matukio yaliyopatikana wakati na baada ya uchaguzi mkuu, jambo lililoifanya Mahakama kuhitimisha kuwa hauingii ndani ya wigo wa kifungu cha 308 cha CPA.

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo mdogo, Mahakama iliahirisha kikao kwa mapumziko mafupi kufuatia ombi la upande wa Jamhuri lililotaka muda wa kutafakari hatua za kisheria zitakazofuata.utolewa kwa uamuzi huo mdogo, Mahakama iliahirisha kikao kwa mapumziko mafupi kufuatia ombi la upande wa Jamhuri lililotaka muda wa kutafakari hatua za kisheria zitakazofuata.

About The Author

error: Content is protected !!