February 22, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

TAMISEMI kushirikiana na wadau wa sekta ya macho kuboresha huduma

 

KATIBU mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Adolf Ndunguru amesema TAMISEMI ikishirikiana na wadau wa sekta ya macho zitaendelea kuhakikisha miongozo na sera zinazoongoza utoaji wa huduma za macho zinaboreshwa, ili kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo. Anaripoti Apaikunda Mosha, Dodoma … (endelea).

Ameeleza hayo leo tarehe 20 Februari 2025 katika hafla ya uzinduzi wa mpango wa macho imara, ambao utatekelezwa katika halmashauri 16 za mikoa minne ambayo ni Arusha, Singida, Tabora na Manyara, ambao utakaogharimu Sh.Bilioni 4.9 kwa muda wa miaka mitano ya utekelezaji wake.

Kwa upande wake Dk. Rashidi Mfaume amesema kutokana na eneo la afya ya macho kupewa kipaumbele cha chini, TAMISEMI kwa kushirikiana na wizara ya Afya, na wadau mbalimbali imejipanga kuhakikisha huduma za macho zinajumuishwa katika mfumo wa afya ya msingi ili kuwafikia watoto wengi kwenye jamii.

Dk. Ziada Sellah naye, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, amesema inakadiriwa kuwa katika watoto 10,000 wenye umri wa kuanzia miaka 0 mpaka 15 kuna wastani wa watoto nane wenye ulemavu wa kutokuona na idadi kubwa zaidi wana upungufu wa kuona.

“Serikali itaendelea kuboresha huduma za uchunguzi wa macho na kutoa afua sahihi kwa watoto tangu wakiwa tumboni mwa mama zao hadi wanapofika umri wa miaka mitano, kwani kipindi hiki ni muhimu sana na ndio matatizo mengi yanayo sababisha ulemavu wa kutokuona kutokea,” amesema Dk. Sellah.

Naye, Daktari Bingwa wa macho kutoka Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Milka Mafwiri amesema lengo la mpango huo ni kupunguza ulemavu wa kutokuona kwa Watoto hapa nchini kwa kuwa watoto milioni 1.4 duniani, wanakabiliwa na tatizo la kutoona huku nusu ya idadi hiyo wakiwa ni Watoto wanaoishi katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

About The Author

error: Content is protected !!