February 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Anuani za makazi kuboresha huduma za kijamii

 

JERY William Silaa, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, leo tarehe 6 Februari 2025 amefanya ufunguzi wa maadhimisho ya kwanza ya Wiki ya Anwani za Makazi nchini ambayo kwa mwaka huu Kitaifa yanafanyika Jijini Dodoma. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo inayosema” TAMBUA NA TUMIA ANWANI ZA MAKAZI KURAHISISHA UTOAJI NA UPOKEAJI WA HUDUMA”

Slaa amesema kuwa anuani ya makazi ni muunganiko wa taarifa na miundombinu ambayo kwa pamoja inatambulisha anwani halisi ya kitu au mtu alipo ili kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma.

Amesema kuwa kwa kutambua hilo Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na wadau wengine hususan Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaratibu utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi nchini.

” Hatua hii ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003; makubaliano ya Kikanda na Kimataifa kupitia Umoja wa Posta Afrika (PAPU) na Umoja wa Posta Duniani (UPU),na Ibara ya 61(m) ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025.

“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila nyumba, jengo, kiwanja, huduma, ofisi ama eneo la biashara linatambulika kwa Anwani ya Makazi, ,anwani ya Makazi inaundwa na Namba ya Anwani maarufu kama namba ya nyumba,Jina la Barabara au Mtaa na Postikodi.

“Postikodi ama nchi zingine zinaita Zipcode ni utaalamu wa kugawa maeneo ili kurahisisha utambuzi. Kwa hapa Tanzania mgawanyo huu umefanyika katika ngazi ya kata ambapo kila Kata ina Postikodi yake yenye tarakimu tano,” amesema Slaa.

Amesema kuwa anwani za Makazi inarahisisha utoaji na upokeaji wa huduma mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya Kiuchumi na kijamii hasa katika zama hizi ambazo Mapinduzi ya 4,5 na 6 ya viwanda yanategemea matumizi ya TEHAMA. Na matumizi ya TEHAMA yanalazimu kuwa na mifumo ya utambuzi ndiyo sababu ya Serikali kuanzia mfumo huu.

Alisema kwamba Itakumbukwa kwamba utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ulianza mwaka 2010 na kwa mujibu wa Mpango wa utekelezaji ulitakiwa ukamilike mwaka 2015 hata hivyo, utekelezaji wake ulikuwa wa kasi ndogo ukilinganisha na matarijio, hali iliyosababisha kuanzishwa kwa Operesheni maalumu iliyojulikana kama Operesheni Anwani za Makazi ambayo ilizinduliwa na Rais, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 08 Februari, 2022. Operesheni hiyo ilifanyika nchi nzima na kusimamiwa na wakuu wa mikoa Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Tamisemi Dk.Festo Ndugange amesema kuwa uwepo wa mfumo wa anuani za makazi ni urahisishaji wa upatikanaji wa huduma kidigitali zaidi.

Aidha amesema kuwa kwa sasa mfumo wa anuani za makzi zimeonesha mafanikio makubwa kwa urahisishaji wa huduma mbalimbali za kijamii ambazo zimekuwa zikionekana kuwa ngumu kupatikana au kuchelewa.

About The Author

error: Content is protected !!