UDASA waichambua hotuba ya Jaji Chande
JUMUIYA ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA), imetoa tamko ikitaja mchanganyiko wa wizi wa mali za umma, uongo wa viongozi, na vitendo vya utekaji kuwa ndivyo vilivyolipua bomu la machafuko ya Oktoba 2025.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Kupitia uchambuzi wa “Jicho la UDASA,” wasomi hao wameibua kero 53 zinazothibitisha kuwa amani haiwezi kurejeshwa kwa mtutu wa bunduki ikiwa viongozi wanaendelea kujitajirisha huku raia wakitekwa na kupotezwa.
​UDASA imesema kuwa imani ya wananchi imeporomoka kutokana na wizi wa kimfumo, ambapo viongozi wamegeuka wezi wa rasilimali za umma na kuishi maisha ya anasa huku wananchi wakikosa ajira na huduma za msingi.
Wasomi hao wamekemea mmomonyoko wa maadili ambapo viongozi wanatoa taarifa za uongo mbele ya umma na kuonyesha kiburi, hali iliyosababisha mifumo ya huduma kama hospitali na ajira kufeli kutokana na ubadhirifu na upendeleo uliokithiri.
​Kuhusu usalama, tamko hilo limeweka wazi kuwa majeraha ya kitaifa yalisababishwa na ongezeko la utekaji nyara huku Jeshi la Polisi likituhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi badala ya kulinda raia.
UDASA imebainisha kuwa Mahakama na Tume ya Uchaguzi zimepoteza uhuru wake, jambo lililowafanya wananchi kuhisi nguvu yao ya kikatiba imepokwa na “wezi wa kura,” hali iliyozua hofu na hasira kubwa miongoni mwa vijana na jamii kwa ujumla.
​Mwenyekiti wa UDASA, Dk. Elgidius Ichumbaki, amesisitiza kuwa suluhu pekee ni Serikali “kujishusha na kukiri makosa yake” kuanzia sasa. Wasomi hao wametoa wito wa kuanzishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya, kuwashitaki viongozi wabadhirifu, na kukomesha utekaji mara moja, wakionya kuwa bila haki, maumivu ya wananchi yataendelea kuwa bomu linalosubiri kulipuka wakati wowote.