Odero Charles Odero
ODERO Charles Odero, amekiri kuona barua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), iliyomfuta uanachama ndani ya chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, Odero amesema, “Nimeona barua, ingawa sijakabidhiwa rasmi.”
Alipoulizwa amepanga kuchukua hatua gani, kurejesha uanachama wake, Odero amesema, “Ninasubiri Jumatatu, kwa kuwa leo Jumamosi na kesho Jumapili, siyo siku ya kazi, ili niweze kuwasiliana na mwanasheria wangu, nitajua cha kufanya.”
Akaongeza, “Nafikiri nitaziarifu mamkala za serikali, kwa kuwa kuna masuala yangu binafsi yameguswa.” Alipotakiwa kutaja masuala yake binafsi ni yapi, Odero aliishia kusema, “Ni taarifa zinazonihusu mimi.” Hakuzitaja.
Odero amekuwa kwenye msuguano wa wazi na baadhi ya viongozi wake, kufuatia uamuzi wake wa kujipa kazi ya kusaidia Serikali kutafuta anachoita, “Maridhiano ya kisiasa,” kwa njia ya kukandia Chadema, kupitia cheo kipya alichojibandika cha Balozi wa Maridhiano.
Kutoka na matendo hayo, Odero amejikuta akilaumiwa kila kona na baadhi ya wanachama na viongozi wa chama hicho, kwamba anachochea mifarakano na kupandikiza migogoro; “kujenga makundi chonganishi na kuhujumu Chadema,” mambo yanayokemewa vikali na katiba ya chama hicho.
Odero ambaye amejipatia umaarufu baada ya kugombea uenyekiti wa taifa wa Chadema, mwishoni mwa mwaka jana, hasa kutokana na kauli yake mbiu ya “Mbele kuna Mwanga,” alitangazwa kuvuliwa uanachama wa chama hicho, kupitia tawi lake la Olosiva, Kata ya Oloirien, jimboni Arumeru Magharibi, mkoani Arusha.
Taarifa ya chama hicho, iliyotolewa jana Ijumaa na tawi hilo, imeeleza kuwa Odero amefutwa uanachama kuanzia juzi, Alhamisi ya 24 Aprili mwaka huu.
Kwa mujibu wa barua yenye Kumb. Na. CDM/ARM/OLO/ODERO/3 ya tarehe 23 Aprili 2016 uamuzi huo umefikiwa baada ya Odero kushindwa kushirikiana na chama chake, licha ya kupewa taarifa na kuitwa kujibu tuhuma zilizokuwa zikimkabili.
Chadema wanasema, mtuhumiwa huyo, aliandikiwa barua mbili zikimtaka kufika kwenye kikao halali cha tawi lake, kilichokutana kwa kuzingatia katiba ya Chadema ya mwaka 2006 (Toleo la 2019), lakini aligoma kuitikia wito huo.
“…ndugu Odero amekiuka masharti ya Ibara ya 5.3.3 na 5.3.4 zinazohusu nidhamu na maadili ya wanachama. Kutokana na ukiukwaji huo, tawi limetumia mamlaka yake kwa mujibu wa Ibara ya 7.2.11(e) pamoja na Ibara ya 5.4.3 kumvua rasmi uanachama kuanzia tarehe ya barua hiyo,” imeeleza. Taarifa hiyo.
Hata hivyo, barua hiyo imebainisha kuwa Odero ana haki ya kukata rufaa kulingana na taratibu za chama kama zilivyoainishwa kwenye katiba ya Chadema.