June 22, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

ACT Wazalendo walia kufungwa kwa Kanisa la Gwajima

 

KUTOKANA na taarifa ya kufutwa kwa usajili wa kanisa la ufufuo na uzima linalosimamiwa na askofu Josephat Gwajima na taarifa ya kukamatwa kwa baadhi ya waumini chama cha ACT Wazalendo kimeitaka serikali kubatilisha uamuzi wake. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … (endelea).

Msimamo huo umetolewa leo tarehe 3 Juni 2025, na Shangwe Ayo, Naibu Katibu wa Uenezi wa Chama cha ACT Wazalendo, na kudai hatua hiyo kuwa ni ya kikandamizi na inavunja misingi ya uhuru wa maoni na uhuru kukusanyika na kuabudu, na inalenga kuzima sauti zinazopinga maovu nchini.

“Tunaitazamia hatua ya serikali ya CCM dhidi ya askofu Gwajima kama muendelezo wa ukandamizaji na ukiukwaji wa haki na uhuru wa maoni pamoja na uhuru wa kuabudu…” amesema Shangwe.

Chama hicho pia kimetoa wito kwa jamii kuungana pamoja kupinga na kukemea vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vilivyoshika kasi ndani ya nchi hasa vitendo vya utekaji, kupotea kwa watu na mauaji.

“Tumeshuhudia viongozi wa makanisa mbalimbali wakitoa kauli na mahubiri ya kuisifia na kuipamba serikali na viongozi wa serikali waziwazi bila kificho. Ikiwa mahubiri ya kuwapamba viongozi wa serikali hayachukuliwi kuwa ni kuchanganya dini na siasa, inakuwaje mahubiri yanayowakosoa na kuwataka kuwajibika kwa wananchi ndio yawe ni uchochezi na kuchanganya dini na siasa?”

Pia wamesema chama kitaendelea kutekeleza wajibu wake kama chama cha siasa kinachotumikia maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha wanapinga vitendo visivyokubalika.

About The Author

error: Content is protected !!