
WAKAZI wa Mitaa ya Mahomanyika, Mahomakulu na Ipala kata ya Nzuguni Jijini Dodoma wamemuomba Rais Samia kuingilia kati mgogoro wa ardhi kati ya wakazi hao na Jiji kwa kitendo cha jiji kutaka kuwapora maeneo yao. Anaropoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea)
Wananchi hao Wakizungumza kwa nyakati tofauti na vyombo vya habari katika eneo la mgogoro wamesema kumekuwepo mgogoro wa miaka mingi wa kutaka kuporwa ardhi yao bila kupewa maelezo yoyote au uelezwa eneo hilo wanatakiwa kulipisha kwa matumizi gani na wanatakiwa wakazi hao kwwnda wapi.
Mzee Daniel Mnyolwa (86) amesema kuwa anasikitishwa na kitendo cha uongozi wa Jiji kwa kitendo cha kuwatuma wapima kwenda kupima ardhi hiyo bila kuwashirikisha wananchi wa eneo husika.
Akielezea kuwepo kwa wananchi katika eneo hilo Mzee Daniel amesema kuwa eneo hilo ni la asili na wamezaliwa na kulikuta na kuliendeleza hadi ambapo nao wana watoto,wajukuu na vitukuu.
“Mimi ni mzee kwa sasa nina miaka 86 nimezaliwa katika eneo hilo wakati huo vikiwa vijiji,tumekua na kuoa na kupata watoto,wajukuu na vitukuu alafu tunaambiwa hapa tumevamia.
“Tunajua kuwa ardhi ni ya serikali na serikali ni siai inakuwaje tunajiwa na polisi wakiwa na mabunduki kwani sisi tupo wapi Kongo au Tanzania na je Serikali ni nani kama siyo sisi kwa hili tunaomba Rais Samia tusaidie kwa maana hapa kuna mchezo na Mungu anaona kilio chetu,” ameeleza Mzee Daniel.
Naye Jane Bwanakoo mkazi wa eneo hilo amesema kuwa anaomba Rais Samia kuingilia mgogoro huo na kuupatia ufumbuzi kwa kuwa wanaoathirika zaidi ni akina mama na watoto.
Amesema kuwa mgogoro huo ambao kwa sasa unazidi kukua na kuwafanya wananchi kukosa amani na kuna uwezo wa kutokea uvunjifu wa amani jambo ambalo halipendezi.
“Sisi hatuna shida na upimaji shida yetu ni kwanini hatushirikishwi na kwanini tunapohoji tunapigwa na kukamatwa na hatufunguliwi kesi,mimi.ni kati ya watu ambao nimeisha pigwa na kuwekwa ndani lakini baada ya kuachiwa sikuelezwa kosa langu wala kupelekwa mahakamani kutokana na hali hiyo inatusukuma kumuomba Rais kuona namna ya kutusaidia kama anavyosaidia watu wengine,” ameeleza Jane.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mahomanyika, Abraham Aizaki amesema kuwa kilio cha wananchi wake ni kuona wanapewa maeneo yao kwa usalama bila kuwepo kwa Mtutu wa Bunduki.
Kiongozi huyo amesema tatizo hilo ni la muda mrefu na limekosa ufumbuzi kwani ni kama linahusisha pande tatu ambazo ni Jeshi,Jiji na wanachi jambo ambalo linasababisha sintofahamu.
Hata hivyo amesema kuwa kinachowachanganya wananchi hadi kufikia hatua ya kupaza sauti na kumpigia magoti kwa Rais ni ili asikie kilio chao ni kutokana na suala la Jiji kutaka kupima maeneo hayo bila kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika.
“Rais ni kiongozi wa wqnanchi wetu sisi wote na anaongoza maskini na matajiri wanyonge na wenye furaha na ni sisi watu wa Chama cha Mapinduzi hivyo tunaomba asikie kilio chetu na atusaidie kama anasaidia wakazi wa maeneo mengine sisi hatutaki migogoro ila tunahitaji haki,” ameeleza Mwenyekiti.
Hata hivyo siku chache baada ya malalamiko ya wananchi alipotafutwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dk. Frederick Sagamiko ili aweze kulitolea ufafanuzi jambo hilo,alisema kuwa hayupo ofisini bali atafutwe siku ya jumatatu ambayo ni tarehe 3 Machi 2025.
Alipofutwa ofisini kwakwe hiyo siku alieleza kuwa hayupo ofisini yupo kwenye vikao na ofisi ameikaimisha kwa Kimaro na alipotafutwa Dikson Kimaro alisema kuwa yupo nje ya ofisini naye amemkaimisha Afisa habari wa Jiji ambaye ni Denis Gondwe.
Kwa upande wake Gondwe alipotafutwa ofisi kwake kwa kupigiwa simu hakuwepo ofisini kwake na badala alisema ana wageni mpaka hatakapomalizana nao hata hivyo hakueleza walikuwa wageni wa serikali au binafsi.
ZINAZOFANANA
Mwenezi Bawacha ashambuliwa mlinzi, Polisi wafunguka
GF Automobile, NaCoNGO zasaini makubaliano ya kimkakati
Hatua za msajili analenga kuinyamazisha ajenda ya Chadema