October 16, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Baa la njaa laikumba Sudan

 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema nchi ya Sudan iliyokumbwa na vita inakabiliwa na njaa ‘kila mahali.’ Inaripoti Mitandao ya Kimataifa, Khartoum, Sudan

Bosi huyo wa WHO ameyasema hayo alipozungumza na mwandishi wa BBC, Mishal Husain, kwenye kipindi cha BBC Today, baada ya kuzuru nchi hiyo.

“Hali nchini Sudan inatisha sana… idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao – sasa ni kubwa zaidi duniani na bila shaka kuna njaa,” amesema Dk. Tedros alimwambia.

Amesema watu milioni 12 tayari wamekimbia makazi yao, akiongeza kuwa jumuiya ya kimataifa haikuweka umakini katika kushughulikia mzozo wa Sudan.

Maelfu ya watu wameuawa tangu kuzuke vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo Aprili 2023 kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha (RSF).

“Fikiria uharibifu, watu kuhama, magonjwa kila mahali, na sasa njaa,” Dk. Tedros amefafanua.

Amesema hivi karibuni alitembelea kambi ya wakimbizi wa ndani na hospitali moja nchini Sudan na kukutana na watoto wengi waliodhoofu kiasi cha mifupa kuonekana.

Kwa mujibu wa Dk. Tedros, takriban watu milioni 25 ambao ni nusu ya wakazi wa Sudan, wanahitaji msaada.

“Sudan haipati uangalizi unaostahili na ndivyo ilivyokuwa kwa migogoro mingine barani Afrika.Hasa katika Afrika, nadhani umakini ni mdogo sana…inasikitisha kwa sababu unaona mara kwa mara, sio tu nchini Sudan,” aliongeza.

About The Author