Mapema leo 20 April 2026,uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) umefanya kikao na ujumbe wa African Women Leaders Network uliokuwa ukiongozwa na aliyekuwa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, akishirikiana na aliyekuwa Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde, waliopo nchini Tanzania kwa ziara maalum. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea). Ziara ya viongozi hao inalenga kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo vyama vya siasa na asasi za kiraia, kwa lengo la kukusanya na kufuatilia taarifa kuhusu matukio yaliyojitokeza kabla na baada ya tarehe 29 Oktoba 2025. Katika kikao hicho, ujumbe wa Chadema uliongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche, akisaidiana na Katibu Mkuu John Mnyika, pamoja na Naibu Katibu Mkuu Bara Amani Golugwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Wakili Ali Ibrahimu na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Suzan Lyimo. Akizungumza katika kikao hicho, uongozi wa chama uliwasilisha msimamo rasmi wa Chadema kama ulivyoazimiwa na Kamati Kuu, ukieleza kwa kina madai ya kuwepo kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na vitendo vya ukatili vinavyodaiwa kutokea kabla, wakati na baada ya tarehe hiyo. Aidha, chama kimesisitiza umuhimu wa kufanyika kwa uchunguzi huru na wa haki ili kubaini ukweli wa matukio hayo, huku kikitaka uwajibikaji kwa wote watakaobainika kuhusika. Pamoja na hayo, Chadema imeeleza kuwa ni muhimu kulinda misingi ya demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria ili kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa nchini. Share this… Facebook Pinterest Twitter Linkedin Whatsapp About The Author Fedrick Gama See author's posts Post navigation Afikishwa kizimbani kwa ulaghai wa milioni 60