LUHAGA Mpina aliyekuwa mgombea wa nafasi Urais kupitia Chama cha ACT Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa 2025 amekutana na mjumbe wa Jumuiya ya Madola kuhusu mgogoro wa uchaguzi wa Tanzania wa mwaka 2025, Lazarus Chakwera, na kueleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya demokrasia nchini.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea). Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika 16 Aprili 2026, Mpina alisema Tanzania ipo katika njia panda ya kihistoria, akidai kuwa matumaini ya mageuzi ya kisiasa yamegeuka kuwa mateso na ukandamizaji. “Tuliahidiwa mwanzo mpya wa kidemokrasia, lakini kilichoshuhudiwa ni kuvunjwa kwa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na kuzimwa kwa sauti za wananchi,” alisema. Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa 2025, Mpina hakusita kuutaja kama batili, akisema haukuwa huru wala wa haki. “Uchaguzi ule haukuwa uchaguzi bali ulikuwa mradi wa kisiasa uliopangwa kuondoa ushindani na kulazimisha matokeo yaliyokusudiwa kabla hata wananchi hawajapiga kura,” alisisitiza. Mpina pia alieleza kuwa kuzuiwa kwake kugombea urais licha ya kukidhi vigezo vyote ni ishara ya kuporomoka kwa demokrasia. “Kuzuiwa kwangu hakukuwa shambulio dhidi yangu binafsi, bali ni kunyang’anywa haki ya mamilioni ya Watanzania kuchagua kiongozi wanayemtaka,” alisema, akituhumu taasisi za uchaguzi kuhusika katika hatua hiyo. Kuhusu mhimili wa Mahakama, Mpina alisema umeshindwa kusimama imara kulinda haki za wananchi. “Haki inapocheleweshwa hupoteza maana yake. Mahakama haiwezi kudai uhuru wake huku ikinyamaza mbele ya ukiukwaji wa Katiba,” aliongeza. Aidha, alizungumzia madai ya ukatili wa dola dhidi ya waandamanaji wa amani, akisema hali hiyo haiwezi kuvumilika. “Matumizi ya risasi dhidi ya wananchi wasio na silaha ni uhalifu mkubwa. Kila aliyehusika lazima awajibishwe hakuna aliye juu ya sheria,” alisema kwa msisitizo. Katika hitimisho lake, Mpina alitoa wito wa hatua za haraka kuchukuliwa ili kurejesha demokrasia nchini. “Mustakabali wa Tanzania hauwezi kujengwa juu ya damu ya wasio na hatia na ukandamizaji. Tunahitaji ukweli, uwajibikaji na mfumo huru wa kidemokrasia sasa, si kesho,” alihitimisha. Share this… Facebook Pinterest Twitter Linkedin Whatsapp About The Author Fedrick Gama See author's posts Post navigation Tanzania na kenya zatajwa ukandamizaji dhidi ya raia nje ya nchi-ripoti Chadema kufanya mkutano wa hadhara nchi nzima