BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono maendeleo ya kiuchumi ya Zanzibar kupitia ufadhili wa miradi mikubwa ya kimkakati ya miundombinu, baada ya kuunga mkono ujenzi wa Kituo cha Abiria cha Vivuko cha Maruhubi (Mpiga Duru) kupitia mkopo rafiki. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Ukamilishwaji wa kituo hicho unatarajiwa kuimarisha sekta za utalii, biashara na usafirishaji katika visiwa hivyo.
NBC, ikiwakilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Wateja Wadogo na Wakubwa, Elibariki Masuke, leo ilishiriki katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, hafla iliyoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah.
Kituo cha Abiria cha Vivuko cha Maruhubi kinajengwa kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kati ya Shirika la Bandari Zanzibar na Kampuni ya Zanzibar Ferry Development Company Limited.
Mradi huu unalenga kupunguza msongamano katika Bandari ya Malindi na kuboresha ufanisi wa usafiri wa abiria, ambapo baada ya kukamilika, kituo kinatarajiwa kuhudumia takribani abiria 8,000 kwa siku, sawa na karibu abiria milioni tatu kwa mwaka.
Kituo hicho cha kisasa kitahudumia vivuko vya abiria, vivuko vya kasi, meli za Roll-on/Roll-off pamoja na teksi za baharini. Pia kitajumuisha eneo la bidhaa zisizotozwa ushuru (duty-free), maduka ya rejareja, marina na kituo cha ndege za baharini (seaplane), hatua itakayoiimarisha Zanzibar kama kitovu cha kikanda cha usafiri wa baharini na utalii.
Mradi huo unakadiriwa kugharimu takribani dola za Marekani milioni 400 na utatekelezwa kwa awamu mbili ndani ya kipindi cha miaka mitatu, huku Benki ya NBC ikiwa miongoni mwa wafadhili wakuu wa mradi huo.

Akizungumza pembezoni mwa hafla hiyo, Masuke alisema NBC inajivunia kuunga mkono mradi unaoendana na vipaumbele vya maendeleo ya Zanzibar.
“NBC inajivunia kuwa benki ya kwanza kutoa msaada wa kifedha kwa mradi huu. Mwezi Februari 2024, tulitoa ufadhili wa mpito (bridge financing) kusaidia utekelezaji wa Awamu ya Kwanza A,” alisema, akiongeza kuwa benki hiyo pia itaunga mkono uendeshaji wa mradi kupitia mifumo ya kidijitali ya ukusanyaji wa mapato katika vituo vya Maruhubi na Malindi, hatua itakayoongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji.
Alibainisha kuwa ushirikiano kati ya NBC na Zanzibar Ferry Development Company ulianza rasmi mapema mwaka 2024, kufuatia kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya kampuni hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 2023, yenye lengo la kuendeleza vituo vya kisasa vya abiria na mizigo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Zanzibar Ferry Development Company Limited, Jaffer Machano ilipongeza jitihada hizo za benki ya NBC, akieleza kuwa ni muhimu katika kusukuma mbele utekelezaji wa mradi huo.
“Tunaishukuru sana Benki ya NBC kwa ufadhili wake mkubwa na ushirikiano wa kimkakati katika mradi huu Kituo cha Abiria cha Vivuko cha Maruhubi. Msaada wa mapema wa NBC na uendelevu wake umechangia kwa kiasi kikubwa kuusogeza mradi huu mbele, na tunatarajia ushirikiano wa muda mrefu utakaotoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Zanzibar,” alisema Machano.
Hivi karibuni, Benki ya NBC pia ilikuwa Mwezeshaji Mkuu na Meneja wa mkopo wa dola za Marekani milioni 200 kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, unaolenga kufadhili miradi mikubwa ya kijamii na kiuchumi.
Kwa sasa, benki hiyo inaendesha matawi mawili Zanzibar pamoja na zaidi ya mawakala wa kibenki 200 katika visiwa hivyo, ikiendelea kupanua huduma zake za kifedha kwa lengo la kuunga mkono maendeleo jumuishi ya uchumi.
ZINAZOFANANA
Badilisha kila mzunguko kuwa fursa ya kushinda na Meridian Mission
NBC yang’ara Tuzo za Mwajiri Bora Programu ya Mafunzo kwa Vitendo
Meridianbet yaongeza thamani ya Win&Go kupitia 10% Cashback