December 21, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

TCB yataja mikakati kuendana na mageuzi ujio wa SGR

 

KATIKA kuwa sehemu ya mradi wa reli ya kisasa (SGR), Benki ya TCB imeeleza kujivunia kuwa benki mdau namba moja katika mradi huo wa kimageuzi kwa kuwezesha mchakato wa kuagiza vichwa vya treni na mabehewa ya SGR na kutoa mikopo kwa wakandarasi wa Yapi Merkezi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumzia mikakati ya benki hiyo katika mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Adam Mihayo amesema lengo lake ni kuhakikisha kwamba wateja wanafikiwa na kunufaika na huduma za mradi wa SGR kupitia mawakala 7000 walioenea nchi nzima.

Pia amesema uwezo mkubwa wa programu maalumu ya TCB Popote, wanamwezesha kila mmoja kujionea urahisi na uhakika wa usafiri huo wa kisasa.

Aidha, Mihayo amefafanua kuwa benki hiyo ilishinda zabuni ya kutoa huduma za ukusanyaji wa nauli kwa njia za kidijiti ikiwemo kupitia mashine za kukatia tiketi (Ticket Vending Machine) ilihali programu ya simu ya TCB Popote inayomwezesha mteja kujifungulia akaunti kwa kiasi cha Sh. 1,000 ikimrahisishia ukataji wa tiketi za SGR mahala popote nchini.

“Wateja pia, wanaweza kununua tiketi zao bila usumbufu kwa mawakala 7000 wa Benki ya TCB waliopo nchi nzima, na hivyo kurahisisha upatikanaji wa tiketi na hivi sasa kadi za ATM zinaweza kutumika katika mifumo ya PoS na mashine za kukatia tiketi (TVM) zilizopo katika stesheni zote,” amesema.

Mihayo amesema katika kuwezesha mfumo kufanya kazi kwa ufanisi, Benki ya TCB imezindua mfumo wa malipo wa QR code kwa abiria ili kuwawezesha kutumia mfumo wa PoS bila kuhitaji intaneti kuzuia makosa ya kimfumo.

Aidha, ubunifu wa mfumo wa kimawasiliano unaotumia akili mnemba kupitia mtandao wa WhatsApp unawezesha upatikanaji wa huduma za SGR kwa urahisi na kwamba, makusanyo ya manunuzi ya tiketi yameunganishwa na mfumo wa GePG ili kuendelea kukuza pato la nchi.

Hayo yanajiri wakati kipande cha mradi huo kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma kikiwa kimekamilika na safari za Dar- Morogoro hadi Dodoma zikianza.

Akihutubia katika uzinduzi huo jijini Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan aliuelezea mradi huo kuwa kielelezo cha maendeleo makubwa ya miundombinu ya Taifa kwa ujumla na kwamba kuanza kwa mradi wa SGR ni hatua muhimu katika kutimiza ndoto ya kuwa na miundombinu ya usafiri wa haraka, rahisi na wa kuaminika.

Alifafanua kwamba matokeo ya mradi yanaweza yasionekane mapema, lakini lengo la mradi ni kutoa huduma kwa Taifa na mchango wake katika kuwezesha biashara za kimataifa na maendeleo ya nchi.

About The Author

error: Content is protected !!