October 16, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NFRA kununua tani milioni 1.7 za nafaka

 

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umesema kuwa umepanga kununua tani 1,750,000 za nafaka mbalimbali kutoka kwa wakulima nchini kwa ajili ya mauzo ya ndani na nje ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma …(endelea).

Kati ya tani hizo, NFRA tayari imeshasaini mkataba wa kuuza tani 1,150,000 katika nchi za Jamhuri ya Congo (DRC) na Zambia na zilizobaki ni kwa ajili ya soko la ndani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana Jumatano, Mkurugenzi Mkuu wa NFRA, Dk. Andrew Komba amesema tani 650,000 za mahindi zimeshaanza kusafirishwa kwenda nchini Zambia tangu wiki iliyopita baada ya malipo kufanyika.

Amesema kuwa tani nyingine 500,000 zimenunuliwa na Serikali ya Congo (DRC) kwa ajili ya jimbo la Katanga nchini humo.

Amesema mbali na kuuza nafaka hizo nchini DRC na Zambia, NFRA pia ipo katika utekelezaji wa mkataba wa kuiuzia nafaka Shirika la Chakula Dunia (WFP) ambazo wanazipeleka nchini Malawi.

Amesema WFP waliomba kuuziwa tani 100,000 lakini wameanza na mkataba wa kuchukua tani 35,000 kwa sasa.

Mkurugenzi Mkuu wa NFRA, Dk. Andrew Komba

“Hii inaonyesha hitaji kubwa la nafaka kwa mwaka huu kwa ajili ya mauzo ya ndani na nje ya nchi na tumejipanga vizuri kukidhi mahitaji ya soko hilo,” amesema Dk. Komba.

Katika hatua nyingine,Dk. Komba amesema kuwa NFRA ina mpango wa kununua tani 600,000 za mahindi na mpunga kutoka kwa wakulima katika utaratibu wake wa kawaida wa kuhifadhi chakula na baadae kukiingiza katika mzunguko.

Kati ya tani hizo, tani 500,000 ni za mahindi na tani 100,000 ni za mpunga.

Amesema ununuzi wa nafaka hizo ni kwa ajili ya usalama wa chakula ambapo tani 500,000 ni za Mahindi na zilizobaki ni za mpunga.

“Lengo ni kuiwezesha nchi kuwa na hifadhi ya kutosha ya chakula. Lakini pia kuziuza nafaka hizo kwa wananchi wenye mahitaji pale watakapohitaji,” amesema.

NFRA ipo imara na itekeleza matarajio ya Serikali inalenga kumkomboa mkulima kwa kununua mazao yao kwa bei nzuri na furahia matunda ya kazi yao na kuongeza kipato.

About The Author