February 17, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali yaanza mpango wa kurasimisha upya wamachinga

 

Serikali imesema inatarajia kuanzisha mfumo utakaowawezesha wafanyabiashara wasio rasmi kutambuliwa ili kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya kodi kwa maendeleo ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mpango huo unalenga kuwahusisha wafanyabiashara hao katika mfumo rasmi wa uchumi na kuongeza mchango wao katika kuongeza mapato ya serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha kikundi kazi cha fedha cha Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Natu El-maamry Mwamba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kikundi kazi hicho, amesema kuwa mpango huo unalenga kuhakikisha kila mfanyabiashara anarasimiwa na kutambuliwa kama mlipa kodi ili kuongeza wigo wa mapato ya serikali.

“Miongoni mwa majukumu ya kikundi hiki ni kuishauri serikali juu ya mikakati ya kupanua wigo wa kodi na kuongeza ukuaji wa uchumi, hasa katika sekta za kimkakati.

“Tunatazamia pia kupunguza viwango vya riba katika masoko ya fedha, hususani riba za mikopo kwa sekta binafsi, ili kuvutia ukuaji wa uchumi na kuibua vyanzo vipya vya fedha,” amesema Dk. Mwamba.

Dk. Mwamba ameongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha kuwa mazingira ya biashara yanakuwa rafiki na wezeshi, huku ikiongeza idadi ya walipa kodi, ikiwemo wale walioko nje ya sekta rasmi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti mwenza kutoka Sekta Binafsi, Theobald Sabi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), amesema kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa Mkutano wa 15 wa TNBC hivi karibuni.

Amesisitiza umuhimu wa kikundi kazi hicho kuendelea kukutana kila robo mwaka ili kutafuta suluhu kwa changamoto zinazowakumba wafanyabiashara na kuibua fursa mpya.

“Katika kikao hiki, tutaendelea kujadili kwa kina changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na kuja na mapendekezo yatakayoleta manufaa kwa Watanzania na taifa kwa ujumla,” amesema Sabi.

Naye Katibu Mtendaji wa TNBC, Dk. Godwill Wanga, ameeleza kuwa Baraza la Taifa la Biashara ni chombo cha juu cha majadiliano nchini, wajumbe wake wakiwa ni viongozi wa kitaifa, mawaziri na viongozi wa sekta binafsi.

Dk. Wanga pia amesisitiza umuhimu wa kurasimisha biashara na kupunguza viwango vya kodi kwa kuongeza idadi ya walipa kodi, hatua itakayopelekea kupungua kwa viwango vya kodi.

Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Sauda Msemo amesisitiza kuwa kukamilika kwa Mfumo wa Jamii Namba kutasaidia kuongeza kasi ya watu kutambulika rasmi katika shughuli za kifedha, hivyo kukuza uchumi na kuweka msingi wa maendeleo endelevu.

“BoT inaendelea kushirikiana na taasisi nyingine za serikali kuhakikisha tunafikia malengo ya kuwa na jamii namba kwa kila Mtanzania. Kupitia kikundi kazi hiki, tutafuatilia kwa karibu ili kufikia malengo yetu,” amesema Msemo.

About The Author

error: Content is protected !!