Mwenyekiti ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman
CHAMA cha ACT Wazalendo kimesema safari ya kuitafuta haki ya uchaguzi inaendelea. Lakini papohapo, kingependa kuona Mahkama Kuu ya Zanzibar inaachiwa kutimiza majukumu yake kwa “uhuru kamilifu.” Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Kupitia Mwanasheria Mkuu wake, Omar Said Shaaban, ACT “kingependa sana” kuona Mahkama iko huru na Serikali inaachia uhuru wa taasisi hiyo ambayo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar jukumu lake kuu ni kutafsiri sheria na kutoa haki inakostahili kisheria, ifanye kazi yake pasina kupokea maelekezo.
Mbele ya waandishi wa habari jana, Mwanasheria Omar aliwaambia kuwa hapo mbele, itakapokuwa uamuzi wa kesi nane za mwisho za uwakilishi umetolewa, tarehe 15 mwezi ujao, wakati itakuwa umefika wa chama hicho kuonesha namna haki inavyozuiwa kutendeka mahkamani.
“Tunaona serikali hii isivyotaka haki ya uchaguzi ijulikane na wananchi. Tulipoamua kufungua mashauri haya mahkamani tulikuwa na maana kubwa. Tunaona mambo yanayotokea. Na upande wetu tuna mafanikio kwa kila hatua tunayopitia kufuatilia kesi hizi. Tutaendelea kutumia njia za kisheria kupigania haki ya watu wetu,” alihitimisha.
Tarehe 22 Aprili, mwaka huu, Jaji Salma Ali Hassan alimaliza usikilizaji wa pingamizi dhidi ya maelezo ya walalamikaji na kupanga tarehe 15 mwezi ujao {Mei} kuwa siku ya kutoa uamuzi. Pingamizi zenyewe zinafanana na zilizokuwa kwa kesi tisa za awali ambazo ziliamuliwa na Jaji Mohamed Ali Mohamed Shein.
Akitoa msimamo huo, Mwanasheria Omar anasema tayari maamuzi ya kesi tisa za awali za uwakilishi yalionesha kuziba nafasi ya mahkama kusikiliza hoja za walalamikaji ili, baada ya kusikiliza pia maelezo ya walalamikiwa, ikiwemo kuona vielelezo mbalimbali vya pande mbili husika, ipime kama malalamiko yaliyowasilishwa mbele yake, yanao au hayana uzito.
“Tutaendelea kutumia njia zote za kisheria pamoja na kanuni za mwaka 2025 za uendeshaji wa kesi za uchaguzi kwenye Mahkama Kuu Zanzibar mpaka tufike mwisho. Kwetu ACT, kila hatua ya kesi hizi ni ushindi… tunayaona tuliyoahidiwa kutoka upande ule, na tunashuhudia yanayotokea pale tunapoomba sisi haki mahkamani na wanapoomba wenzetu,” alisema.
Anazungumzia namna kanuni za usikilizaji mashauri ya uchaguzi zinavyokiukwa, akitaja kupita siku 30 tangu kuwasilishwa rufaa mara mahkama ilipotoa uamuzi wa kuziondoa kesi lakini ukakuta rufaa haijasikilizwa.
Mwanasheria Mkuu Omar anasema wamepokea samansi inayotaka wafike mahkamani tarehe 7 mwezi ujao kwa ajili ya usikilizaji wa rufaa kuanza kupitia jopo la majaji watatu.
Hatua ya awali ya kesi hizo ilipokamilika, ilikuwa ni jukumu la kikatiba la Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla kupanga majaji wa kuzisikiliza. Alizipanga kesi tisa kusikilizwa na Jaji Shein na kesi nane kumpangia Jaji Salma.
Jaji Shein aliamua kuziondoa kesi kwa kuridhia hoja za wanasheria wa upande wa walalamikiwa – Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar {ZEC} na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar – kwamba viapo vya waombaji vina kasoro za kisheria ikiwemo madai kuwa wakili aliyeapisha hajapata kibali cha kusimamia viapo mwaka huu.
Viapo vya walalamikaji ambao ni wanachama wa ACT Wazalendo vilisimamiwa na Wakili maarufu na mzoefu nchini, Jaji mstaafu Ussi Khamis Haji. Uamuzi huo ulimsukuma kumwandikia Mrajis wa Mahkama Kuu, Valetino Katema kulalamikia uamuzi huu. Anajieleza kuwa yeye alitimiza wajibu wake ipasavyo na anayo stakabadhi ya malipo ya kuhuisha kibali ya tangu Disemba mwaka 2024.
Wakati Mwanasheria Mkuu Omar anasema wamepokea samansi kuwa rufaa zitatajwa tarehe 7 Mei 2026 mbele ya majaji Rabia Hussein, Said Hassan Said na Jaji Salum aliyeko kisiwani Pemba, kesi zilizoko Pemba hazijafika makao makuu ya Mahkama ya Zanzibar iliyopo Tunguu, kisiwani Unguja, ili zimfikie Jaji Mkuu ambaye inatarajiwa ateue majaji wa kuzisikiliza. Rufaa hizo ziliwasilishwa mahkamani mwanzoni mwa mwezi Machi.
Mbali na uwakilishi, ACT pia ilifungua kesi za kupinga uchaguzi wa wabunge katika majimbo 33. Kesi 19 kwa majimbo ya Unguja na 14 majimbo ya Pemba. Hata hivyo, kesi zote hizo zimeamuliwa kwa kuondolewa mahkamani baada ya Jaji Haji Suleiman Haji Tetere kuridhia pingamizi zilizowasilishwa na upande wa walalamikiwa wakidai Mahkama Kuu ya Zanzibar haina uwezo wa kisheria wa kusikiliza kesi zinazohusu uchaguzi wa wabunge.
Rufaa za kupinga uamuzi huo Mahakama ya Rufaa Tanzania zimeshawasilishwa lakini Mwanasheria Mkuu Omar anasema bado hawajapokea wito wa Mahkama hiyo kuonesha zimepangiwa jaji wa kusikiliza.