Uhuru wa habari Tanzania uko hatarini-CoRI
UMOJA wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) umetoa tamko zito ukilaani mwenendo unaoendelea wa baadhi ya viongozi wa serikali, taasisi za umma, na vyombo vya usalama kudhoofisha uhuru wa wanahabari nchini, hali ambayo imetajwa kuwa “inatisha.”Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Katika tamko lililotolewa leo 28 Aprili 2026, jijini Dar es Salaam, umoja huo umebainisha kuwa ndani ya miezi minne tu ya kwanza ya mwaka huu, tayari matukio manane ya madhila yamesharipotiwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Manyara, Mbeya, na Mwanza, yakihusisha ukamataji wa waandishi, kutaifishwa kwa vifaa vya kazi, na kufungiwa kwa chombo cha habari kwa siku 90.
​Mwenendo huu wa hali ya uhuru wa vyombo vya habari kwa mwaka 2026 unaonyesha kutokuwepo kwa mabadiliko makubwa kulinganisha na mwaka jana, jambo linaloashiria kuendelea kwa mazingira magumu ya utendaji kazi kuelekea kilele cha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari hapo 3 Mei 2026.
CoRI imesisitiza kuwa jumla ya matukio 55 ya madhila yameandikwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita, hali inayochochea hofu na tabia ya wanahabari “kujidhibiti” (self-censorship), jambo ambalo ni pigo kubwa kwa uwazi, uwajibikaji, na ujenzi wa demokrasia imara nchini.
​Licha ya Tanzania kuonyesha maendeleo katika viwango vya Kimataifa vya Uhuru wa Habari (RSF) kwa kushika nafasi ya 95 mwaka 2025, umoja huo umeonya kuwa kuendelea kwa matukio haya kunaleta taswira hasi kwa Taifa na kudhoofisha jitihada za serikali katika kuhamasisha uhuru wa kujieleza.
CoRI imebainisha kuwa bila vyombo huru vya habari, michakato ya kisiasa na utawala bora hutetereka, hivyo kuathiri haki ya wananchi kupata taarifa sahihi na kwa wakati ili kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
​Kufuatia hali hiyo, CoRI imetoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha ulinzi wa wanahabari na kuvitaka vyombo vya dola kuacha mara moja vitendo vya vitisho na unyanyasaji.
Umoja huo, unaojumuisha taasisi kama TEF, MCT, LHRC, na THRDC, umesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mdau, ikiwemo mamlaka za udhibiti, kuhakikisha sheria zinatumika kwa haki ili kulinda uhuru wa habari ambao ndio nguzo kuu ya uwazi na utawala wa sheria katika jamii yoyote ya kidemokrasia.