Tabia ya kunyamazisha maoni yaibuka, wajumbe wa tume wapokea matusi zaidi ya 300
MJUMBE wa Tume ya Uchunguzi wa ghasia zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi, Profesa Ibrahim Juma, amesema kuna dalili hatari ya kuibuka kwa tabia ya baadhi ya watu kutaka kuzima maoni ya wengine na kulazimisha mitazamo yao pekee kusikilizwa.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumanne 28 Aprili 2026, Profesa Juma amesema hali hiyo imejitokeza wazi hata baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya tume hiyo, ambapo baadhi ya wajumbe wamekumbana na wimbi la matusi kupitia simu zao.
Amesema jumla ya ujumbe zaidi ya 300 wa matusi umetumwa kwa baadhi ya wajumbe wa tume, hatua anayoitafsiri kuwa ni jaribio la kuwanyamazisha na kuzuia maoni yaliyokusanywa kupitia mchakato rasmi wa utafiti kuwafikia wananchi.
“Baada ya kutoa taarifa tumepokea matusi zaidi ya 300 kwa sababu kuna watu hawataki maoni yetu, yaliyopatikana kwa kutumia mbinu za kisayansi za kusikiliza wananchi, yafikie umma,” amesema Profesa Juma.
Ameonya kuwa mwenendo huo unaweza kudhoofisha misingi ya majadiliano ya kidemokrasia na uhuru wa kujieleza, akisisitiza umuhimu wa kuheshimu tofauti za maoni katika kujenga taifa lenye mshikamano na utulivu.