Watanzania watakiwa kuendelea kushikamana
TAMASHA la Usiku wa Mtanzania limegeuka kuwa jukwaa muhimu la kuikumbusha jamii thamani ya umoja na mshikamano huku Makamu wa Rais Emmanuel Nchimbi akitoa wito kwa watanzania kuendelea kushikamana katika miaka 62 ya Muungano.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Nchimbi alisisitiza kuwa mshikamano wa kitaifa si chaguo, bali ni wajibu wa kila Mtanzania katika kuenzi misingi iliyowekwa na waasisi wa Muungano Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume.
Nchimbi alisisitiza kuwa dira ya uongozi wa sasa chini ya Samia Suluhu Hassan inaweka mbele umoja, amani na mshikamano kama nguzo kuu za maendeleo ya taifa huku akiwataka hasa vijana kujitafakari na kuchukua nafasi yao katika kuulinda Muungano huo uliodumu kwa zaidi ya nusu karne.

“Ni muhimu kujenga utamaduni wa kuvumiliana, kusikilizana na kukubaliana hata pale tunapotofautiana mawazo,” alisisitiza Nchimbi, akiongeza kuwa nguvu ya taifa ipo katika umoja wake.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Yussuf Masauni, alisema tamasha hilo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mshikamano kati ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Masauni ampongeza Rais Samia pamoja na Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, kwa hatua kubwa iliyopigwa katika kushughulikia changamoto za Muungano, akibainisha kuwa hoja 22 kati ya 25 zimepatiwa ufumbuzi hatua inayozidi kuimarisha misingi ya Muungano huo.
Alieleza pia kuwa maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano yameambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo uzinduzi wa miradi ya maendeleo, makongamano na midahalo ya kitaifa, yote yakilenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa Muungano.