KATIKA hatua inayoashiria mwelekeo mpya wa soka la Tanzania, mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya NBC, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), kwa kushirikiana na Azam TV wamezindua rasmi kipindi kipya cha uchambuzi wa soka kiitwacho “Kona ya NBC”—jukwaa la kisasa litakalounganisha burudani, maarifa na fursa za kiuchumi kwa wadau wa mchezo huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Uzinduzi huo wa kihistoria ulifanyika jana jioni jijini Dar es Salaam, ukihusisha wadau mbalimbali wa soka akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Cornel Barnabas, Meneja wa Mahusiano ya Umma wa Azam Media, Christina Korosso, wachambuzi wa michezo, wanahabari pamoja na wachezaji wa zamani na wa sasa, wakiwakilishwa na kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Nassor Saadun.

Hafla hiyo ilirushwa mubashara kupitia Azam TV, huku wageni wakipata fursa ya kuishuhudia kupitia skrini kubwa ndani ya ukumbi wa kisasa wa sinema wa Century Cinemax uliopo Mlimani City—taswira halisi ya namna teknolojia na burudani zinavyoungana kuleta uzoefu mpya kwa mashabiki.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alisisitiza kuwa uwekezaji wa benki hiyo kwenye soka unaenda mbali zaidi ya udhamini wa kawaida—unalenga kujenga mfumo endelevu wa kiuchumi unaonufaisha wadau wote wa mchezo huo.

“Kupitia ‘Kona ya NBC’, tunapanua wigo wa thamani katika soka—kuanzia kwa wachezaji, vilabu, vyombo vya habari hadi wafanyabiashara wadogo na wakubwa. Huu ni uwekezaji unaolenga ajira, ubunifu na ustawi wa vijana,” alisema Sabi.

Aliongeza kuwa tangu mwaka 2023, NBC imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 32.6 katika maendeleo ya soka, ikiwa ni pamoja na udhamini wa Ligi Kuu ya NBC, ligi daraja la kwanza na ligi za vijana—hatua iliyochochea ushindani, uimara wa kifedha wa vilabu na kuongezeka kwa hamasa ya mashabiki.

Akionyesha matumaini yake, Sabi alitolea mfano wa mataifa makubwa ikiwemo Ujerumani ambao kupitia ligi yao maarufu ya Bundesliga ikiwa na dhana inayofahamika kama “football tractor effect”, soka limekuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji uchumi likitumika kuvutia ukuaji wa sekta nyingine kama utalii, biashara, vyombo vya habari, na ajira.

“Lakini pia sote ni mashahidi jinsi ambavyo ligi Kuu ya Uingereza yaani English Premeier League inavyotumika kuimarisha uchumi wa nchi hiyo. Tumeona Ujerumani, tumeona Uingereza. Sasa ni wakati wa Tanzania. Yes, why not us?’’ alihoji Sabi.

Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano ya Umma wa Azam Media Christina Korosso alieleza kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuinua ubora wa maudhui ya michezo nchini.

“Kupitia ‘Kona ya NBC’, Azam TV tunaleta jukwaa la kisasa linalounganisha wadau wa soka—kuanzia uwanjani hadi majumbani. Lengo ni kuongeza ubora wa maudhui, ushiriki wa mashabiki na kukuza tasnia ya michezo kwa ujumla,” alisema.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Cornel Barnabas aliipongeza NBC kwa mchango wake mkubwa katika mageuzi ya soka la Tanzania, akieleza kuwa uwekezaji huo unaendelea kufungua milango mipya ya fursa kwa vijana na kuimarisha nafasi ya soka katika uchumi wa taifa.

“Uwekezaji wa NBC unaendelea kuleta mageuzi makubwa katika soka letu. Sio tu unaongeza ushindani wa ligi, bali pia unafungua fursa kwa vijana na kuimarisha mchango wa soka katika uchumi wa taifa. Uzinduzi wa Kona ya NBC ni hatua muhimu katika kuendeleza mafanikio haya,” alisema Barnabas.

Kipindi cha “Kona ya NBC”, ambacho kitarushwa kupitia Azam Sports HD 1 kila Jumatatu saa 1:00 jioni na kurudiwa Jumanne, kinatarajiwa kuwafikia zaidi ya watazamaji milioni 14 kila wiki.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Masoko wa Benki ya NBC, David Raymond, mbali na uchambuzi wa kina wa mechi, kipindi hicho kitajikita pia katika simulizi za mafanikio, majadiliano ya fursa za kiuchumi ndani ya michezo, pamoja na kuwapa mashabiki nafasi ya kushiriki na kutoa maoni yao.

“Kwa kuwa mpira wa miguu ni miongoni mwa burudani zinazopendwa zaidi nchini Tanzania, tunaamini kipindi hiki kinakwenda kutoa jukwaa madhubuti la kuifikia jamii kwa urahisi, huku kikitoa burudani na kuelimisha masuala ya kifedha.’’ Alibainisha Raymond.

Kwa mashabiki, hiki si kipindi cha kawaida—ni darasa jipya la kujifunza namna ya kunufaika na soka nje ya uwanja. Baadhi yao wameeleza matarajio makubwa wakiamini kuwa jukwaa hili litavunja dhana ya muda mrefu ya kushabikia bila kunufaika.

“Hiki ni kipindi kitakachotufungua macho. Kwa muda mrefu tumekuwa mashabiki tu, sasa tunakwenda kujifunza namna ya kunufaika kiuchumi kupitia mchezo tunaoupenda,” alisema Shabiki wa Yanga SC maarufu kwa jina la God Yanga kauli iliyoungwa mkono na mwenzake kutoka klabu hasimu ya Simba SC.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!