Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Nchimbi awataka Mabalozi wateule kuimarisha Uhusiano ya Kimataifa

MAKAMU wa Rais Balozi Emmanuel Nchimbi amewasihi Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika Mataifa mbalimbali kutanguliza mbele maslahi ya Taifa ya kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia. Anaripoti mwandishi wetu, Dar es Salaam …(endelea).

Balozi Nchimbi amesema hayo, wakati akizungumza na Mabalozi wateule wanaokwenda kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mataifa mbalimbali, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma kwa lengo la kuwaaga mabalozi hao.

Nchimbi amewaasa mabalozi hao kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni pamoja na kutangaza fursa zilizopo nchini na kuwashawishi wawekezaji na wafanyabiashara kuwekeza nchini na kuimarisha uhusiano wa kimataifa.

Aidha Nchimbi amewaagiza Mabalozi hao kuhakikisha wanasimamia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na miongozo mbalimbali kutoka Serikalini.

Nchimbi amewapongeza Mabalozi hao kwa kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenda kuiwakilisha nchi katika Mataifa mbalimbali na kuwasihi kutumia vema imani hiyo waliyopewa.

Kwa upande wake Balozi Mteule wa Tanzania nchini Oman Balozi Maulidah Hassan amemshukuru Makamu wa Rais kwa muongozo, maelekezo na ushauri aliyotoa na kuahidi kufanya kazi kwa bidii.

Mabalozi hao wateule waliofika kwaajili ya kuaga kabla ya kwenda kwenye vituo vyao ni pamoja na Balozi Mhandisi Zena Ahmed Said (Saudi Arabia) Balozi Cyprian Luhemeja (Zambia),Balozi Maulidah Hassan (Oman),Balozi Salim Othman Hamad (Comoro),Balozi Swahiba Mndeme (Sweden),Balozi Noel Kaganda (Korea) na Balozi Musa Haji Ali, Naibu Mwakilishi wa Tanzania Umoja wa Mataifa, New York.

About The Author

error: Content is protected !!