Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Tume ya 29 Oktoba yakutana na Rais Chakwera

 

RAIS mstaafu wa Malawi, Dk. Lazarus Chakwera, leo Jumamosi, tarehe 11 Aprili 2026, amefanya mazungumzo na Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya 29 Oktoba 2025. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari, muda mfupi baada ya Dk. Chakwera, kukutana na tume ya Rais ya 29 Oktoba, mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mkuu mstaafu Othuman Chande, amesema kuwa tume yake, imekutana na ujumbe huo, “kutokana na maelekezo ya serikali.”

Kwa mujibu wa Jaji Chande, mazungumzo kati ya tume ya Rais na Dk. Chakwera, yalijikita zaidi katika kueleza shughuli za tume pamoja na hadidu zake rejea zinazoongoza utekelezaji wa majukumu yao.

Dk. Chakwera aliyewasili nchini Tanzania juzi Alhamisi, ametumwa na katibu mkuu wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth), Shirley Botchwey, kuja kuchunguza matukio ya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu, yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.

Sektarieti ya Jumuiya ya Madola, imemteuwa Dk. Chakwera, kuja nchini kushughulikia mgogoro huo wa kisiasa na kuanzisha mjadala jumuishi kuhusu maridhiano, haki za kisiasa na kuimarisha demokrasia.

Tayari amekutana na makundi mbalimbali, ikiwamo chama kikuu cha upinzani nchini (Chadema), ACT-Wazalendo na baadhi ya mashirika ya kiraia.

Dk. Chakwera ameongoza na naibu katibu mkuu wa jumuiya hiyo, Prof. Luis Franceschi. Anatarajiwa kuondoka nchini, tarehe 16 Aprili.

Matokeo ya majadiliano kati ya mjumbe maalum aliyetumwa na Commonwealth na serikali ya Tanzania, pamoja na wadau wengine nchini, yatatumika kuishauri Jumuiya ya Madola kuhusu hatua itakayofuata kupitia jukumu lake la diplomasia ya “Good Offices.

“Dk. Chakwera anatajwa na wachambuzi wa mambo kuwa ana uzoefu mkubwa katika maeneo hayo. Kabla ya kuwa rais, alikuwa kiongozi wa upinzani.

Uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana ulitawaliwa na vurugu, ambazo mashirika ya kimataifa, vyombo vya habari vya nje na Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, wanasema kwamba waliouawa ni maelfu.

Jaji Warioba alifika mbali zaidi kwa kusema, waliouwa kwenye maandamano hayo, wamezidi waliokufa kwenye vita vya Kagera. Hakutaja idadi yao.

About The Author

error: Content is protected !!