Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mutungi akutana na Chakwera

Spread the love

 

MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amekutana kwa mazungumzo na Dk. Lazarus Chakwera, mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola nchini Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, haikutaja kilichozungumzwa na viongozi hao wawili. Waliishia kusema, “lengo la kikao hicho, lilikuwa kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kisiasa na kiutawala.”

Hata hivyo, MwanaHALISI Online linazo taarifa kuwa Dk. Chakwera, yuko nchini kwa kazi maalum ya kuchunguza kilichosababisha machafuko ya wakati wa uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba mwaka na jinsi ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka makao makuu ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth), nchini Uingreza, mwakilishi wa katibu mkuu, aliyewasili nchini jana Jumatano, anatarajiwa kukutana na makundi mbalimbali, vikiwamo vyama vya siasa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.

Vyanzo vya taarifa vinasema, mikutano hii ya Dk. Chakwera, ni hatua ya mwanzo ya majadiliano kuhusu masuala yanayohusiana na uchaguzi na mustakabali wake.

Katika ziara hiyo, atakutana na viongozi wa serikali, wanasiasa, mashirika ya kiraia, viongozi wa dini na mila, pamoja na wadau wa kitaifa na kimataifa.

Mazungumzo hayo yanapania kuanzisha mjadala jumuishi kuhusu maridhiano, haki za kisiasa na kuimarisha demokrasia.

Jumuiya ya Madola ilianza mchakato wa kusaidia juhudi za maridhiano nchini Tanzania, mara baada ya kutokea machafuko yaliyosababisha mauaji ya mamia ya raia, wanaodaiwa kupigwa risasi na vyombo vya usalama na miili yao kutopatikana.

Katibu mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Botchwey, alianza kushughulikia mgogoro wa kisiasa nchini, Novemba mwaka jana na kwamba Dk. Chakwera alitarajiwa kuwasili Tanzania tarehe 18 Novemba mwaka jana.

Lakini ziara hiyo, ilikwama baada ya serikali ya Tanzania kutompa ushirikiano, jambo lililosababisha Jumuiya ya Madola, kutishia kuifukuza uanachama.

About The Author

error: Content is protected !!