VIONGOZI wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamekutana na Mjumbe aliyetumwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola nchini, Dk. Dk. Lazarus Chakwera, leo Ijumaa, tarehe 10 Aprili. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Rais wa zamani wa Malawi, yuko nchini Tanzania, kuongoza ujumbe wa Jumuiya ya Madola, kushughulikia mgogoro wa kisiasa, uliotokana na uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba mwaka jana.
Taarifa iliyotolewa na chama hicho kwa umma, imeeleza kuwa msafara wa Chadema uliokwenda kukutana na Dk. Chakwera, uliongozwa na makamu mwenyekiti wa chama hicho, John Heche.
Wengine waliokuwamo kwenye msafara huo, ni Dk, Rugemeleza Nshala, mwanasheria mkuu wa chama hicho; John Mnyika, katibu mkuu, Amani Golugwa, naibu katibu mkuu-Bara; Suzana Lyimo, mwenyekiti wa baraza la wazee la Chadema (BAZECHA) na Jenerali Twaha Ulimwengu, rafiki wa Chadema.
Dk. Lazarus Chakwera, aliwasili nchini juzi Jumatano, amekuja nchini kufuatilia matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na mauaji ya raia, yaliyoripotiwa kutokea tarehe 29 Oktoba.
Katika kikao hicho, Dk. Chakwera amepokea taarifa ya msimamo wa Kamati Kuu (CC) ya Chadema, iliyoeleza kwa kina matukio ya kabla na baada ya 29 Oktoba mwaka jana.
Mengine waliyojadili, ni kukamatwa kwa mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, pamoja na wimbi kubwa la utekaji, utesaji na mauaji, pamoja na kuzuiliwa kwa shughuli halali za kisiasa za Chadema.
Aidha, Chadema imewasilisha ombi maalum kwa Dk. Chakwera na kwenda gerezani kumuona Lissu, anayeshikiliwa kwa kesi ya uhaini.
Chadema kimemtaka rais mstaafu wa Malawi, kufika Gereza Kuu la Ukonga, ili kujionea mwenyewe maisha halisi ya Lissu gerezani humo na hali halisi aliyonayo kwa ujumla.
Mwakilishi wa katibu mkuu wa Commonwealth, ameanza mikutano yake kwa kukutana na makundi mbalimbali, vikiwamo vyama vya siasa na mashirika ya hiari.
Mikutano ya Dk. Chakwera, inatajwa kuwa ni hatua muhimu ya kujenga majadiliano juu ya masuala yanayohusu uchaguzi na maridhiano ya kitaifa.
Matokeo ya majadiliano hayo, yatatumika kuishauri Jumuiya ya Madola kuhusu hatua itakayofuata kupitia jukumu lake la diplomasia ya “Good Offices.”
“Hatua hii ni muhimu kwa taifa ambalo linataka kuanza safari ya kutafuta maridhiano ya kitaifa na kuimarisha misingi ya kisiasa, kijamii na kimaendeleo,” ameeleza afisa mmoja wa Jumuiya ya Madola, ambaye hakupenda kutajwa jina lake.
Maandamano ya siku tatu, kuanzia 29 Oktoba 2025, yameacha doa kubwa nchini Tanzania.
Watu kadhaa wameripotiwa kupoteza maisha, wengine kujeruhiwa na uharibifu mkubwa wa mali za umma na binafsi ukifanyika, zikiwamo ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
ZINAZOFANANA
ACT-Wazalendo yampa mazito Chakwera
Mutungi akutana na Chakwera
Mwaka mmoja wa Lissu gerezani