February 18, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Lissu alivyombana shahidi wa 11 neno kwa neno

Tundu Lissu akiwa mahakamani

 

TUNDU Lissu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anaendelea kujitetea huku akijua kuwa kwenye kesi hiyo ya uhaini inayomkabili katika Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam akitiwa hatia atahukumiwa kunyongwa. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Lissu ameendelea kujitetea kwa kumuuliza maswali ya dodoso shahidi wa 11 wa serikali ambaye ni wa kificho aliyepewa utambuzi wa P7.

Kesi hiyo inayosikilizwa mahakamani hapo na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akishirikiana na Jaji James Karayamaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.

Lissu: Tarehe 3 Aprili uliandika maelezo?

Shahidi P7: Waliandika.

Lissu: Tarehe 3 Aprili uliandika maelezo ya kwamba wewe ulitaka kufanya fujo kweli au sio kweli?

Shahidi P7: Kweli.

Lissu: Yako wapi?

Shahidi P7: Mimi sio polisi hayo maelezo yameandikwa na polisi.

Lissu: Tarehe 17 Aprili uliandika maelezo kweli au sio kweli?

Shahidi P7: Kweli.

Lissu: Naomba aoneshwe maelezo yake ya tarehe 17 Aprili 2025?

Shahidi anapelekewa maelezo yake.

Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama ni maelezo yako?

Shahidi P7: Nimeyatambua ni yangu.

Lissu anamsomea maelezo shahidi kuhusu mazungumzo yao kwenye kijiwe cha bodaboda kwa Mrombo jijini Arusha ambapo alipodai kuwa waliona video ya Lissu akihamasisha kuzuia uchaguzi maelezo hayo yalieleza kuwa wakiwa watu wengi walijadili hotuba hiyo ya Lissu na namna walivyokamatwa na Polisi.

Lissu: Sasa shahidi pahala ambapo umesema pamekosewa ulisema ni mwaka wako wa kumaliza shule ya msingi, hapa pameandikwa ulimaliza mwaka 2009, wewe unasema ulimaliza 2014 ukitoa hayo yote ni ya kwako.

Shahidi P7: Ndio

Lissu: Naomba uwaeleze majaji kama ungependa maelezo yako yapokelewe kama kielelezo cha ushahidi?

Shahidi P7: Ndio.

Jaji Ndunguru anakipa utambuzi wa D10 kielelezo hicho.

Lissu: Naomba shahidi apatiwe kielelezo D10

Lissu: Nataka nikihoji kuhusiana na kielelezo hicho, katika ushahidi wako leo ulieleza pale kwa Mrombo kuna watu wengi wakiwemo kina mama ntiliye, wenye maduka kweli au sio kweli?

Shahidi P7: Kweli.

Lissu: Waeleze majaji kama hayo maneno yapo?

Shahidi P7: Hayapo.

Lissu: Umeeleza kwenye ushahidi wako kwamba ukiwa hapo kijiweni kwa Mrombo, mlikuwa mnazungumza mazungumzo ya kawaida, kweli au sio kweli?

Shahidi P7: Kweli.

Lissu: Na baada hapo akatokea mtu moja alisema maneno hamjasikia kwa Chadema watazuia uchaguzi kweli au sio?

Shahidi P7: Kweli.

Lissu: Waambie majaji kama hayo maneno yapo?

Shahidi P7: Ndio.

Lissu: Onyesha yapo wapi?

Shahidi P7: Hapa imesema kwa ameanzisha lakini ..

Lissu: Umeandika hivi tukiwa kijiweni kwetu ilianzishwa mada ilikuwa inazungumzia kauli za Lissu. Hayo maneno kwamba mtu mmoja alianzisha mada kwamba mmesikia Chadema yapo?

Shahidi P7: Hapana.

Lissu: Umeeleza kwenye ushahidi wako huyo mtu mmoja alisema tena wamesema watakinukisha mbaya?

Shahidi P7: Yapo .

Lissu: Yapo wapi?

Shahidi P7: Watakinukisha.

Lissu: Nikusomee ulichoandika?

Shahidi P7: Soma

Lissu: Umeandika hivi, ilianzishwa mada ingawa sijui nani alianzisha kwamba mmesikia kauli za Chadema kwamba tutakinukisha je kuna mahali umeandika kuwa hayo maneno yalisemwa na mtu mmoja?

Shahidi P7: Hapana.

Lissu: Katika ushahidi wako wa leo umesema hivi huyo mtu mmoja akasema polisi wanaiba kura hata ukienda mahakamani hutapata haki kwa sababu majaji ni vibaraka wa CCM?

Shahidi P7: Kweli.

Lissu: Sasa waambie majaji kwenye maneno yako yapo maneno kwamba ukienda mahakamani hutapata haki kwa sababu majaji ni vibaraka wa CCM?

Shahidi P7: Rudia.

Lissu: Anarudia “hayo maneno yapo?

Shahidi P7: Napitia, “hayapo”.

Lissu: Sasa shahidi ukaendelea kwenye ushahidi wako leo umasema Hivi huyo mtu mwenzesha mada alisema mwaka 2020 tume ya Taifa ya uchaguzi ilikata majina ya wapinzani?

Shahidi P7: Kweli.

Lissu: Waeleze majaji kama hayo maneno yapo?

Shahidi P7: Hayapo.

Lissu: Waeleze majaji kama umetaka Tume ya Uchaguzi hata mara moja kwenye maelezo yako?

Shahidi P7: Hayapo.

Lissu: Waeleze majaji kama katika maelezo yako umetaja habari za uchaguzi wa 2024 hata mara moja?

Shahidi P7: Hamna.

Lissu: Umesahau ulichoandika Polisi?

Shahidi P7: Nilikuwa naandika maelezo sio kitabu.

Lissu: Nani alikufundisha kutoa ushahidi nzuri kama huu?

Shahidi P7: Unamaanisha nini.

Lissu: Sasa shahidi waeleze majaji kama haya maneno kama ulipata hamasa yapo kwenye maelezo yako?

Shahidi P7: Hayapo.

Lissu: Shahidi kwenye maelezo yako leo ulisema kwamba baada ya kusikia hayo maneno kijiweni ikibidi uiingie kwenye simu yako janja kweli au sio kweli?

Shahidi P7: Kweli.

Lissu: Waeleze majaji kama kuna Mahali ulionesha kwamba uliingia kwenye mtandao ya YouTube kwa simu yako janja?

Shahidi P7: Mimi nahisi uliingia kwenye YouTube lazima utatumia simu.

Lissu: Huwezi kutumia Kompyuta?

Shahidi P7: Mimi sina Kompyuta.

Lissu: Sio lazima waeleze majaji kama kwenye maelezo yako umetaja neno simu yako?

Shahidi P7: Sijataja.

Lissu: Sasa shahidi kwenye ushahidi wako ulisema kwamba uliingia mtandao kwenye channel ya Jambo kweli au sio kweli ?

Shahidi P7: Kweli.

Lissu: Waeleze majaji kama kwenye maelezo yako kuna hiyo uliingia mtandao kwenye channel ya Jambo

Shahidi P7: Hapana.

Lissu: Sasa shahidi twende kwenye ushahidi wa baada ya kukamatwa na kupelekwa Polisi Sentro Arusha, ulisema uliingizwa kwenye ofisi ya RCO ukaambiwa unahojiwa kwa kosa la kutaka kufanya fujo kweli au sio kweli?

Shahidi P7: Kweli.

Lissu: Waeleze majaji kama kuna mahali kwenye maelezo uliandika kama mnashtakiwa wewe na P4 kwa kutaka kufanya fujo?

Shahidi P7: Ndio.

Lissu: Waeleze majaji kama maneno yapo?

Shahidi P7: Hayapo.

Lissu: Kwa ushahidi wako wa umeeleza kwamba. Hapo kwa RCO uliandika maelezo na kisha ukaingizwa mahabusu mpaka ulivyofuatwa na ndugu zako kesho yake asubuhi na kupewa dhamana kweli au sio kweli?

Shahidi P7: Kweli.

Lissu: Sasa swali langu waeleze majaji kama hayo maneno kwamba ulidhaminiwa asubuhi yapo kwenye karatasi yako ya maelezo?

Shahidi P7: Haipo.

Lissu: Baadala yake ulisema ulidhaminiwa lini soma hayo maneno baada kuhojiwa nikawekwa mahabasu kesho yake mchana nikadhamini au sio?

Shahidi P7: Ndio.

Lissu: Unafundishwa akili ya kutoa ushahidi na mapolisi, sasa tuendelee “kwenye kielelezo hicho shahidi umesema hivi tarehe 3 Aprili ukiwa kijiweni kwa Mrombo ilianzishwa mada kuhusu maneno ya Lissu kwamba mwaka huu tutazuia uchaguzi tutakinukisha kweli au sio kweli?

Shahidi P7: Kweli.

Lissu: Waeleze majaji kama ulitaka huo mtandao?

Shahidi P7: Nimetaja.

Lissu: Wapi?

Shahidi P7: mtandao wa YouTube.

Lissu: Akaunti ya nani ya YouTube umetaja?

Shahidi P7: Sijataja.

Lissu: Waeleze majaji kama katika maelezo yako umetaja akaunti au jina la mtandao wowote iwe YouTube au Instagram ?

Shahidi P7: Ndio nimetaja.

Lissu: Akaunti ya nani?

Shahidi P7: Huwezi akiingia katika YouTube kama huna akaunti.

Lissu: Umasema kama vijana mtakuwa tayari kuungana mkono kwa lolote atakalowaambia Lissu?

Shahidi P7: kweli.

Lissu: Waeleze majaji kama kuunga mkono kauli za Lissu kama ni kosa kwa mujibu wa sheria

Shahidi P7: Mimi sijui maana mimi sio mwanasheria.

Lissu: Waeleze majaji kama ni kosa kuunga mkono kauli za Lissu na chama chake ni kosa kwa sheria?

Shahidi P7: Nishakujibu mimi sio mwanasheria.

Lissu: Mlikuwa mnasisitizana kuunga mkono kauli zangu za kuzuia uchaguzi, kuzuia uchaguzi ni kosa?

Shahidi P7: Ni kosa ndio maana tumekamatwa.

Lissu: Sasa shahidi baada ya kukamatwa mlisema mliandika maelezo na kuambiwa kama mlifanya kosa la kutaka kufanya fujo Waambie majaji kama mlipelekwa mahakamani?

Shahidi P7: Sijapelekwa mahakamani.

Lissu: Waeleze majaji baada kuchukuliwa maelezo yako kama polisi walihangaika tena na ww kuhusu hilo kosa lako?

Shahidi P7: Ndio maana walikuwa wananiambia niliripoti.

Lissu: Wakati unaripoti polisi walikuambia nini?

Shahidi P7: Milikuwa nafagia nje halafu naondoka.

Lissu: Kwa hiyo ilikuwa unaambiwa fagia kisha unaondoka hajakuambia kama utapelekwa mahakamani?

Shahidi P7: Ndio maana nipo hapa.

Lissu: Hapa upo kwa ajili ya kosa langu mimi ?

Shahidi P7: Wewe ndio ulionisababishia

Lissu: Tarehe 17 Aprili mwaka jana uliandika hivi tuliambiwa tusubiri kwa maana tutahojiwa tena?

Shahidi P7: Kweli.

Lissu: Kwanini ulihojiwa tena?

Shahidi P7: Sijui.

Lissu: Waambie majaji kama tuliambiwa unatakiwa uwe shahidi kwenye kesi yangu?

Shahidi P7: Hawajaniambia.

Lissu: Haya uliyoandika yametokana na maswali ya polisi kweli au sio kweli?

Shahidi P7: Hapana.

Lissu: Nani aliyekuwa anakuhoji si polisi?

Shahidi P7: Ndio.

Lissu: Kwa hiyo hayo maelezo yako yametokana na mahojiano na polisi?

Shahidi P7: Ndio.

Lissu: Umekujaje hapa mahakamani?

Shahidi P7: Kwa miguu.

Lissu: Kutoka Arusha mpaka Dar es Salaam umekujaje?

Shahidi P7: Nimepanda basi.

Lissu: Nani alikuambia uje hapa mahakamani?

Shahidi P7: Polisi walinipa summons.

Lissu: Nani alikupa nauli?

Shahidi P7: Mwanamke wangu.

Lissu: Waeleze majaji kama kuna kiongozi yoyote wa Chadema aliyekutishia kukudhuru au kukutishia maisha yako tangu mwezi Aprili mwaka jana?

Shahidi P7: Sijawahi kutishiwa kwa sababu huwezi kutishiwa mtu usiyemjua.

Lissu: Waeleze majaji kama kuna kiongozi au mfuasi wa Chadema ambaye ametishia kuharibu mali yako?

Shahidi P7: Sijawahi kutishiwa.

Lissu: Waeleze majaji kama kuna ndogo yako au rafiki yako amewahi kutishiwa kwa sababu wewe kutoa maelezo polisi?

Shahidi P7: Bro (kaka) maswali yako yanajirudia nimeshakuambia mtu hawezi kukutishia kama hakujui.

Lissu: Kwanini umepewa jina la P7?

Shahidi P7: Kuficha utambulisho wangu.

Lissu: Kwanini?

Shahidi P7: Kwa sababu ya usalama wangu.

Lissu: Sio umesema hujatishiwa?

Shahidi P7: Ndio kwa sababu ya usalama.

Shahidi amehitimisha kutoa ushahidi wake.

Upande wa serikali umeiomba mahakama hiyo kuahirisha shauri hilo kutokana na kuchelewa kwa shahidi wa 12.

Kesi itaendelea kesho saa tatu asubuhi

About The Author

error: Content is protected !!