February 13, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Kesi ya Lissu yaanza kunguruma

KESI inayomkabili mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) – chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania – Tundu Lissu, tayari imeanza kusikilizwa leo, Ijumaa tarehe 13 Februari 2026. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

Upande wa mashitaka umemleta mahakamani shahidi wake wa siri -P6, kutoa ushahidi dhidi ya Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini. 

Mapema kabla ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo, wafuasi na viongozi wa chama hicho, waliofika mahakamani, kufuatilia kesi hiyo, walifanya maombi maalum kumuombea Lissu afya njema, nguvu ya kusikiliza kesi yake na haki kutendeka.

Lissu aliwasili mahakamani, majira ya saa mbili na nusu asubuhi chini ya ulinzi mkali. Katika kesi hiyo, Jamhuri inawakilishwa na jopo la mawakili, wanaongozwa na Nassoro Katuga, pamoja na Renatus Mkude. Mawakili wengine, ni Cathbert Mbiringe.

Yafuatayo, ni mahojiano kati ya Mbiringe na shahidi wake. 

Sahidi wa kificho anaeleza kuwa anatokea mkoani Ruvuma na kazi yake ni Bodaboda. Anajitambulisha kuwa mwanachama wa Chadema, aliyeanza kushiriki siasa mwaka 2024.  

Wakili: Eleza mahakama ulipokuwa kwenye mtandao wa youtube ulikuwa unafanya nini?

Shahidi: Kwenye Youtube niliingia kwenye akaunti ya JAMBO TV.

Wakili: Baada ya kuingia Jambo TV?

Shahidi: Nilifanikiwa kuona video ya hotuba ya mwenyekiti wa chama cha Chadema akiwa anahutubia watu kwamba bila ya mabadiliko hakuna uchaguzi hivyo ‘tunaenda kukinukisha tunakwenda kuvuruga uchaguzi.

Niliona akisema, ‘tunakwenda kukinukisha na yeyote ambaye atakuwa pamoja nasi tutaenda naye ambaye hatotaka tutamuacha.

Pia alisema, ‘kama kuna mtu yeyote anatarajia kugombea udiwani asahau.’ Alisema, ‘yeyote anayetarajia kugombea ubunge pia asahau’ akaendelea kusema ‘hata mimi mwenyekiti kuhusu kugombea urais hilo sahau’ pia akasema ‘bila ya mabadiliko hakuna uchaguzi.’

Wakili: Kingine kipi alisema? 

Shahidi: Alisema ‘watasema tunafanya uasi, ni kweli ni uasi bila ya mabadiliko hakuna uchaguzi.’

Wakali: Alikuwa anazungumza kwenye mazingira gani?

Shahidi: Ilikuwa ukumbini sehemu aliposimama nyuma kulikuwa na bendera ya taifa na bendera ya Chadema pembeni.

Wakili: Lissu alikuwa kwenye muonekano gani siku hiyo.

Shahidi: Alikuwa amevaa kombati ya kaki

Wakili: Huyo Tundu Lissu wewe unamfahamu vipi?

Shahidi: Namfahamu kama mwanasiasa mkongwe na maarufu.

Wakili: Baada ya kuona na kusikia hiyo video nini kilifuata?

Shahidi: Maneno yake yaliniingia na kunishawishi kuwa miongoni mwa wale watakaounga mkono ajenda ya kuzuia uchaguzi pasipo na mabadili.

Wakili: Kuzuia vipi uchaguzi.

Shahidi: kuzia uchaguzi kwa maana ya kukinukisha.

Wakili: Na hiyo ajenda ambayo unasema ulishawishika ni ipi?

Shahidi: Ajenda ya kukunukisha ni kwamba kufanya vurugu au kuharibu uchaguzi.

Wakili: Shahidi umezungumza kuhusu uchaguzi huo uchaguzi ni upi?

Shahidi: Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ambao unahusisha madiwani wabunge na Rais.
Jana kabla ya kesi kuhairishwa kutokana na Lissu kutopewa chakula na maofisa wa magereza, shahidi wa kwanza wa kificho, aliiambia mahakama kuwa alisema kwamba ‘alliona video ya Lissu akisema atakinukisha na uchaguzi mkuu hautafanyika.’

Akaongezea kwamba ‘aliihofia video hiyo ingesababisha uvunjifu wa amani, kukwamisha biashara na kusababishia njaa.

Hata hivyo, akimjibu shahidi huyo, Lissu alisema, Nukisha inatokana na neno nuka na kwamba inaweza kuwa harufu nzuri au harufu mbaya.

Lissu ambaye anajiwakilisha katika kesi hiyo, alimuuliza shahidi huyo kuhusu video aliyokuwa akiitazama Facebook ilikuwa kwenye akaunti ya nani wakati alipokua anaiperuzi.

Shahidi alimjibu akisema hakufahamu kupitia account gani.

Mashahidi wapatao 30 wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

About The Author

error: Content is protected !!