October 24, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Askofu Bagonza atoa somo kwa serikali

Askofu Benson Bagonza

 

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza, ameitaka serikali kuwaheshimu viongozi wa madhehebu ya kidini, ili waweze kuwa na sauti kwa wanaowangoza. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

“Mkitaka viongozi wa dini wasikilizwe na kuheshimiwa na waumini, basi ni sharti serikali ianze kuwaheshimu na kuzingatia maoni yao,” ameeleza.

Anaongeza, “Wananchi wakiona serikali inaheshimu na kuzingatia ushauri wa viongozi wa dini, basi wananchi nao watawaheshimu viongozi wa dini kwa kile wanachoshauriwa.”

Kwa mujibu wa Askofu Bagonza, huwa tunawaambiwa tusinywe pombe, msizini, msitumie uzazi wa mpango. Serikali ndiyo ya kwanza kupuuza tunachowaambia waumini.

Anasema, “kuna viongozi wa dini tulikuwa tunaheshimika kiasi fulani. Tumesukumizwa kwenye matope. Heshima tuliyoijenga muda mrefu, inachafuliwa na hotuba ya dakika tano.

“Huu ni ukatili kwa viongozi wa dini na watu mashuhuri wanaosukumizwa bila utashi ili waseme wasichokiamini.”

Anasema, “Njia nzuri, rahisi, nyepesi na ya gharama nafuu ya kusimamia utawala wa sheria, ni kwa serikali kuheshimu na kufuata utawala wa sheria.”

Anasema, wananchi wakiona serikali inaheshimu sheria kuliko matamko, watafuata na kuheshimu sheria.

“Ukiona ‘hebeas corpus’ (kulazimisha waliofichwa mahabusu kuletwa mahakamani), zimepamba moto, ujue mtunga sheria anavunja sheria,” anaeleza.

Polisi wakiwa mtaani kulinda amani

Anasema, “Miaka yote watu hukamatwa na kufunguliwa mashtaka hata ya uwongo. Hapakuwa na kuteka, kuficha, kukana, kusafirisha kwa kificho na kukanusha ukweli. Tubadilike, tutaona matokeo ndani ya muda mfupi.”

Akizungumzia matumizi ya polisi siku ya kupiga kura, anasema kuwapo magari mitaani siku ya kupiga kura, yana maana mbili za haraka – kuwalazimisha watu kupiga kura na kuwazuia watu kupiga kura.

Anasema, “najua ipo ya tatu ambayo iko vichwani mwa polisi, lakini haiaminiki na watu. Mimi ni mtu, nawaambia yanayosemwa na watu.

“Maandamano hayapo. Polisi ndio wataandamana. Ondoeni polisi mitaani. Kama kuna watakaoandamana, wasindikize bila kuwazuia wanaotaka Kutiki. Huo ni utawala wa sheria, si wa matamko. Uchaguzi utapita, tutabaki,” anaeleza.

Anaongeza: “Siku tukiamka asubuhi tukakuta watu wote wanatiki, wamevaa kijani, wanaimba Bagonza mitano tena, wanasema katiba mpya ilaaniwe, hatutaki tume huru na tunataka chama kimoja tu; siku hiyo hata machawa watakimbia nchi.

Anasema, “Kinachowapa ajira machawa ni tofauti ya maoni. Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni nzuri kwa kuwa kuna Chaumma. Ikibaki peke yake, haitamaniki.”

Anasema: “Tungeheshimu maoni tofauti, hata mwenye shahada ya kupiga kura iliyofutikafutika asingeruhusiwa kupiga kura.

“Tunakoelekea hata asiyejiandikisha atapiga kura ili wawe wengi. Tuache kupigana na maoni ya watu, chaguzi zitaheshimika.”

Kuhusu dhana ya maridhiano baada ya uchaguzi, Bagonza anakopa kauli ya Wajaluo inayosema, “ukiacha nyoka wakati wa kufyeka pori, utamkuta wakati wa kupalilia.”

Dhambi ya makusudi ni kumkufuru roho. Kutenda dhambi makusudi ukipanga kutubu baadaye ni kufuru.

Yaweza kuwa na msamaha wa kibinadamu. Mungu anajijua mwenyewe. Tunamjua kwa sehemu. Tumeshindwa kukemea utekaji, hata kununa tumeshindwa?

Mama mkwe akikuzingua, Mzingue bintiye. Mtaheshimiana. Turudi mezani; hatupotezi, tunapata.

About The Author

error: Content is protected !!