
KIKOSI Kikosi cha Polisi Wanamaji Zanzibar kimepokea boti mpya ya kisasa kwa ajili ya shughuli za doria, operesheni na uokoaji kwenye maeneo ya baharini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Zoezi hilo la makabidhiano limefanyika leo, tarehe 8 Oktoba 2025, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama wa watumiaji wa bahari na mali zao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kamanda wa Kikosi cha Polisi Wanamaji Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Moshi Sokoro, amesema kuwa, boti hiyo pamoja na nyingine mbili zilizotengwa kwa ajili ya mikoa ya Pemba, zinatarajiwa kuongeza ufanisi wa Jeshi la Polisi katika kutekeleza majukumu yake ya kulinda amani na usalama kwenye maeneo ya bahari.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Christopher Fuime, ambaye amepokea boti hiyo kwa niaba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, amesema Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na Taasisi na Wadau wengine kuhakikisha boti hizo zinatumika ipasavyo katika kukabiliana na vitendo vya kihalifu baharini.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Akif Ali Khamis, amepongeza hatua hiyo na kueleza kuwa, uwepo wa boti hizo utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya bandari na maeneo ya mwambao kwa ujumla.
ZINAZOFANANA
Yaliyojiri mahakamani kesi ya Lissu neno kwa neno
Lissu aibua mapya mahakamani
Update kesi uhaini: Lissu ambana shahidi tafsiri ya neno uasi