
MAKUMI ya Watanzania wanaoishi nchini Afrika Kusini, wanafanyiana vitendo vya kikatili, ikiwamo mauaji, utekaji na kulawitiana. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Mohamed Taliban Msangi, Kiongozi wa Watanzania anayeishi Afrika Kusini, ameeleza kuwa vitendo hivyo vimeshamiri nchini humo na Watanzania wenyewe ndio wanaofanyiana vitendo hivyo.
Kufuatia hali hiyo, Msangi, ametaka Watanzania wanaotaka kwenda nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika, kuacha mara moja kufanya hivyo, kutokana na alichokiita, “kushamiri kwa vitendo hivyo.”
Msangi ametoa kauli hiyo, katika mahojiano yake na MwanaHALISI TV, yaliyofanyika jana Ijumaa, jijini Dar es Salaam.
Amesema, “Watanzania waache kwenda kutafuta maisha nchini Afrika Kusini na badala yake wanaweza kubaki nchini mwao au kwenda nchi nyingine kwa kuwa kwa sasa, Afrika Kusini siyo eneo salama.
Amesema, “Afrika Kusini imebadilika sana. Vijana kutoka Tanzania wengi wao wanafanyiana ukatili wa kijinsia na kuuana bila woga. Wamesahau kabisa utamaduni wa hapa nyumbani.
Aidha, Msangi ameitaka serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuboresha mfumo wa ajira ili vijana wajivunie kubaki kwenye nchi yao ya asili, badala ya kukimbilia nchi nyingine kutafuta maisha.

Kwa mujibu wa Msangi, kumekuwepo na malalamiko mengi ya Watanzania katika ubalozi wetu nchini Afrika Kusini, kutokana na madhira yanayowakuta vijana wanaoishi nchini humo.
Anasema, “Kinachowaponza Watanzania pale Afrika Kusini, ni kuishi bila vibali,” hivyo ametumia nafasi hiyo kuwataka kufuata sheria za nchi wanayotaka kuishi.
Katika hatua nyingine, Msangi ameiomba serikali kupunguza adhabu kwa raia wake wanaokamatwa kwa kukosa vibali na kufungwa mara mbili nje ya Tanzania na wanaporudi nchini.
“Huwezi kumpa mtu adhabu mara mbili kwa kosa moja. Ni vema serikali ikaliangalia suala hili viziuri. Hawa vijana hawaondoki kwa kutaka. Wanakwenda nje ya nchi yao, kutokana na kutafuta nafuu ya maisha,” ameeleza.
Januari mwaka huu, serikali iliwafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, raia 55 wa Tanzania ikiwatuhumu kuondoka nchini kwenda Afrika Kusini bila kuwa na kibali.
Tukio hilo, lilidaiwa kulitenda kufanyika 31 Desemba 2024, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA).
Baadaye mahakama hiyo, chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, iliwahukumu kulipa faini ya Sh. 40,000 au kwenda jela miezi sita kila mmoja.
Waliohukumiwa adhabu hiyo katika kesi ya jinai namba 574/2025, ni James Mkadam (31), Shaban Bora (26), Hemed Jongole (25), Mathew Kazoka (45) na David Makota (29) ambaye ni Mhadisi wa programu (Software Engineer), pamoja na wenzao 50.
ZINAZOFANANA
Changamoto za afya barani Afrika zitatatuliwa na CDC
Kesi ya Lissu kuanza kutolewa ushahidi Oktoba 6, Samia atajwa
NBC yaitambulisha Kampeni ya NBC Shambani kwa wakulima wa korosho, mbaazi, ufuta Tunduru