
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele, ametembelea vituo vya uchaguzi, ili kujionea maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa ya tume kwa umma imeeleza kuwa Jaji Mwambegele alitembelea halmashauri ya jiji la Mbeya, lenye majimbo ya uchaguzi ya Mbeya Mjini na Uyole, jana Ijumaa, tarehe 19 Septemba 2025.
Tayari tume imeshawasilisha vifaa vinavyotarajiwa kutumika kwenye uchaguzi huo; Jaji Mwambegele alikagua vifaa vilivyopokelewa katika halmashauri ya jiji la Mbeya.
Aidha, Jaji Mwambegele alipata fursa ya kutembelea kampeni za wagombea ubunge wa Chama cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika majimbo hayo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na tume, uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, unatarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba mwaka huu.
Hata hivyo, hofu imeanza kutanda miongoni mwa jamii, kwamba uchaguzi huo, utakuwa na uhaba mkubwa wa wapigakura.
Ari ya wananchi kupotea kwenye uchaguzi huo, kunatokana na kinachoitwa, “kuenguliwa kwa mgombea urais wa ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina na kutoshiriki kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema.”
Chadema kiliondolewa kwenye uchaguzi baada ya kugoma kusaini kanuni za maadili za uchaguzi, kwa maelezo ya kutoshirikishwa katika uandaji wa kanuni hizo na kutaka kuwapo mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi.
“Pamoja na mamia ya wananchi kuhudhuria mikutano ya kampeni ya chama tawala, bado kuna uwezekano wa watu wengi kujitokeza kupiga kura, ni mdogo mno,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi serikalini.
Sababu nyingine inayotajwa kuwa huenda ikachangia kupunguza wapigakura, ni kauli ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima (Glory of Christ Church), lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam, Josephat Gwajima, kueleza kuwa baadhi ya waumini wake, hawatampigia kura wagombea wa CCM.
Alitoa kauli hiyo, mara baada ya Serikali kupitia kwa msajili wa taasisi za kidini, Emmanuel Kihampa, kufungia kanisa lake. Serikali imemtuhumu Askofu huyo, kutoa mahubiri yanye mwelekeo wa kisiasa na kuchonganisha serikali na wananchi.
Gwajima ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) ya chama tawala na mbunge wa anayemaliza muda wake Kawe, katika jimbo la Kawe.
Katika mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu, ndani ya chama chake, Askofu Gwajima, hakujitosa kutetea nafasi hiyo.
Maeneo yanayotajwa kuwa huenda watu wasijitokeze kwa wingi kushiriki uchaguzi, ni Kanda ya Ziwa Viktoria, kunakodaiwa kuwa bado baadhi ya wananchi wana kinyongo na CCM na wagombea wake.
Maeneo mengine yanayotajwa ni mikoa ya Kaskazini ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara; mkoa wa Singida, Dar es Salaam, pamoja na majimbo yote ambayo yalikuwa ngome ya upinzani.
Maeneo mengine yatakayoathirika, ni majimbo ambayo wabunge waliokuwa wanatetea nafasi zao, wameenguliwa; na au walioshinda kura za maoni ndani ya CCM, siyo waliorejeshwa.
ZINAZOFANANA
Msaidizi wa Mafwele aanza kutoa ushahidi kesi ya Lissu, kesho zamu yake kumbanwa
Hukumu kesi ya Mpina, INEC kutolewa Alhamisi
Lissu asimamisha mahakama kisa tarehe ya hukumu yake kabla ya kusikilizwa