August 9, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Kanisa Katoliki latangaza siku ya mfungo

KANISA Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, limewaagiza Madekano, Maparoko, Watawa na Waamini wote Walei, kutekeleza agizo lililotolewa na Askofu Mkuu Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, kufunga Novena ya kuliombea taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa ya Jimbo Katoliki Dar es Salaam, iliyosainiwa na Pd. Vincent Mpwaji, imesisitiza kuwa “Mhashamu Askofu Mkuu ameagiza kwamba katika Parokia zote na Asasi zote katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ifanyike Novena ya siku tisa (9) kuomba Haki na Amani kuanzia tarehe 15 hadi 23 Agosti 2025.”

Amesema, Askofu Mkuu ameelekeza kwamba Novena hiyo iambatane na kuabudu Ekaristi Takatifu, Kusali Rozari Takatifu na kusali sala ya Kuiombea Tanzania kama iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Ameongeza, “Katika siku ya kilele cha Novena, yaani Jumamosi ya 23 Agosti, ambayo ni kuomba Haki na Amani, sote tunaalikwa kufuata ratiba iliyotolewa na Idara ya Kichungaji ya TEC.

“Ratiba hiyo inaelezea namna ya kufanya sala na mfungo huo ambao utaanza siku hiyo tarehe 23 Agosti kwa adhimisho la Ekaristi Takatifu, ikifuatiwa na kuabudu Ekaristi Takatifu ikiambatana na vipindi mbalimbali vya sala, mafundisho, na ukimya, na kuhitimishwa Dominika tarehe 24 Agosti kwa adhimisho la Misa Takatifu kama inavyoelekezwa katika maelekezo yaliyotoka TEC.”

Maelekezo ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, yameambatanishwa na kinachoitwa, “barua ya TEC na mwongozo wa sala.”

Anasema, uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, unapendekeza kwa Parokia zote, kwamba Misa hii ya hitimisho la mkesha iwe Misa ya kwanza.

“Sala mbalimbali ambazo zimeelekezwa/ zimependekezwa katika ratiba hii iliyotolewa na TEC, tunaweza pia kuzitumia katika kusali Novena iliyoelekezwa hapo juu,” imeeleza taarifa ya kanisa.

TEC limeagiza kufanyika sala maalum ya kitaifa kwa makanisa yake na mafungo, ili kuliombea taifa haki na amani, kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa 2025.

Maaskofu walitoa wito huo kupitia barua yao rasmi ya tarehe 20 Juni 2025. Ilisainiwa na mwenyekiti wa idara yake ya Liturujia, Simon Chibuga Masondole, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda.

Uamuzi wa maaskofu wa TEC ulifikiwa mara baada ya kumalizika mkutano wao mkuu wa 109 uliofanyika Kurasini, jijini Dar es Salaam, kuanzia tarehe 16-19 Juni 2025.

Mkutano wa TEC ulihitimishwa kwa kauli mbiu ya “Taifa linapoendelea na safari katika Tumaini lisiloisha katika mwaka huu Mtakatifu wa Jubilei Kuu 2025.”

About The Author

error: Content is protected !!