
MFANYABIASHARA Mohamed Dewji (MO), anayemiliki Kampuni ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL), amesema anataka kukumbukwa kwa maisha aliyoyabadilisha kwa Watanzania na si kwa si kwa kiasi cha fedha anachokipata kupitia uwekezaji anaoufanya ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Anaripoti Salehe Mohamed, Dar es Salaam … (endelea).
Katika taarifa yake aliyoitoa siku chache tu kupita baada ya kutajwa na jarida la Forbes kuwa ni miongoni mwa matajiri 22 barani Afrika ambao utajiri wao umeongezeka kutoka dola bilioni 82.4 kwa wafanyabiashara 20 mwaka 2024 hadi Dola bilioni 105 mwaka 2025, amesema anaamini mafanikio ni kugusa na kubadilisha maisha ya watu.
Taarifa ya Forbes inaonyesha kuwa utajiri wa MO umefikia zaidi ya dola bilioni 2.3 (Trilioni 4) ambapo umekuwa kati ya dola milioni 400–500 katika kipindi cha mwaka mmoja (2024/2024).
Mo Dewji amesema biashara inaweza kuwa chombo cha mabadiliko chanya—kutoka kujenga viwanda na kuzalisha ajira hadi kusaidia jamii kupitia ufadhili wa programu mbalimbali zinazogusa maisha ya watu kama anavyofanya kupitia Taasisi ya Mo Dewji Foundation (MDF) inayorudisha kwenye jamii kile anachokipata kwa kufadhili masuala ya elimu, maji, afya na mengineyo kulingana na mahitaji ya wananchi.
Mfanyabiashara huyo, ameahidi kutoa nusu ya utajiri wake kwa misaada ikiwa ni kufuata mafundisho ya imani yake ambapo anasisitiza kuwa “Nilifundishwa na wazazi wangu kuwa uhisani ni wajibu, si chaguo.
Mafanikio hayapimwi kwa faida pekee bali yanapimwa kwa athari chanya unazoziacha kwa jamii na kinachopaswa kuzingatiwa ni athari unayoacha kwa jamii, nafasi za ajira unazounda na maisha unayogusa.”
Mfanyabiashara huyo ameeleza kuwa hivi sasa ameamua kuwekeza kwa nguvu zaidi katika maeneo manne anayoamini yana matokeo chanya kwa maisha ya wajasirimali na makundi mbalimbali nchini.
Maeneo ambayo mfanyabiashara huyo anawekeza zaidi ni kwenye sekta za mali isiyohamishika, ukarimu, usindikaji taka na teknolojia ya fedha (FinTech) ambazo anaamini zinakamilisha nguzo alizosimika katika viwanda vya chakula, utengenezaji na biashara ya rejareja.
Taasisi ya Mo Dewji Foundation (MDF), imekuwa mfano wa kuigwa kwa kurudisha kwenye jamii ambapo imefadhili masuala ya elimu, maji, afya na mengineyo kulingana na mahitaji ya wananchi jambo linaloonyesha utu na kuwajibika kwa jamii.
Shughuli za uhisani wa MO zinapanuka zaidi kupitia ushirikiano wa kimataifa na taasisi ya Chuo Kikuu cha Georgetown, MDF inaendelea kuleta athari chanya katika nyanja za afya, elimu, na upatikanaji wa maji safi kwa wale wanaohitaji zaidi.
Mfanyabiashara huyo amesema tangu mwaka 2018, alipopatwa na mkasa wa kutekwa ameongeza kasi ya kupanua biashara zake kimataifa na kujikita zaidi katika ujasiriamali wenye matokeo chanya uliochagiza kuongezeka kwa utajiri wake.
“Sitaweza kufanikiwa kwa kutegemea Afrika pekee, Afrika ni nyumbani, lakini tunastawi pia Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya na sehemu yoyote tunapoona fursa tunaichangamkia ili kuleta uvumbuzi wenye tija,” anasema Mo.
Anasema wajasirimali wa Afrika wanapaswa kuwa na matumaini na kujitegemea na yeye yupo tayari kuisaidia jamii bila kujali mipaka ya kijiografia.
“Nina mapenzi makubwa na Tanzania lakini ni wakati sasa wa dunia kutambua kuwa Afrika inaweza kutoa kampuni kubwa za kimataifa—kampuni na viongozi wenye athari ya kweli duniani kote. Kwa mtazamo sahihi, tunaweza kupeleka maadili yetu ya mshikamano, huruma na ukarimu katika jukwaa la kimataifa,” anasema
Licha ya MeTL Group kujikita Tanzania lakini mafanikio yake yamevuka mipaka kwa muda na chini ya uongozi wa MO, kampuni hiyo imevuka mipaka na kufanya shughuli katika nchi zaidi ya 11 za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
“Kila soko jipya linaongeza mapato ya kampuni, kupunguza utegemezi kwenye uchumi mmoja pekee, kutawala soko la ndani ilikuwa hatua ya kwanza na MeTL imekuwa miongoni mwa kampuni zenye mchango kwenye Pato la Taifa. Dira yetu daima ilikuwa Afrika nzima na hatimaye dunia nzima.”
“Dira hiyo sasa ni ukweli, MeTL inasafirisha bidhaa zake kuanzia nyuzi za mkonge hadi bidhaa za walaji katika masoko ya Mashariki ya Kati, Asia, na Ulaya. Kupitia vituo vyake vya biashara huko Dubai.
“Leo, MeTL ni kampuni yenye nguvu ya Kiafrika yenye uwepo wa kimataifa unaoanzia Kenya, Uganda, Msumbiji, Zambia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, hadi India, Thailand, Italia, Vietnam na kila nchi yenye fursa za biashara” anasema
Mo amewekeza katika viwanda vya nguo na kilimo, ambavyo mara nyingi huepukwa kwa kuonekana ngumu kwa sababu ya hatari zake lakini yeye alifanya hivyo kwa kutambua fursa zilizokuwa hazijatumika na kuwanufaisha Watanzania.
“Aliokoa mashamba ya mkonge yaliyokuwa yameachwa, akieleza kuwa “uzalishaji wa nyuzi za mkonge kwa kiwango kikubwa ni kama kuchapisha pesa, pia alianzisha Mo Cola kushindana na wazalishaji wa kimataifa wa vinywaji baridi sambamba na kuhamasisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa zinazotegemewa kutoka nje” anasema mmoja wa wafanyakazi katika viwanda vyake.
Akizungumzia hatua aliyofikia MO, anasema; “Mafanikio hayapimwi kwa faida pekee bali yanapimwa kwa athari kwa jamii na kinachopaswa kuzingatiwa ni athari unayoacha kwa jamii, nafasi za ajira unazounda na maisha unayogusa.”
Mafanikio kwenye Simba SC
Miongoni mwa mambo anayojivunia MO ni kubadilisha klabu ya Simba kuwa klabu ya kiwango cha juu Afrika ambapo kwa nafasi yake ya rais wa heshima na mwekezaji mkuu, amesimamia mageuzi makubwa yaaliyoifanya timu hiyo kutoka nje ya nafasi 100 bora hadi nafasi ya 7 barani Afrika.
Mabadiliko aliyoyaongoza ni makubwa kutoka kwa mchakato wa kuijengea taswira mpya klabu,kutambulisha nembo mpya na kuhakikisha kuhakikisha wachezaji wanalipwa mishahara rasmi yenye hadhi ya kazi wanayoifanya.
“Mpira si kuhusu kushinda pekee bali kuhusu kuhamasisha vijana na kutoa fursa zinazoleta mabadiliko ya kweli, ninataka nikumbukwe si kwa kiasi cha pesa nilichopata, bali kwa maisha niliyo badilisha,” anasema MO.
ZINAZOFANANA
Wanawake wasiojistiri vyema ni wachafu
Waumini wa Dini ya Kiislamu wapewa mwongozo
Sheikh Ponda: Mifumo ya uchaguzi irekebishwe