February 13, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Polisi wakwama, mwakilishi Wingi aachiwa huru

 

MJUMBE wa Baraza la Wawakilishi, Jimbo la Wingwi, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Kombo Mwinyi Shehe ameachiwa huru na Polisi bila ya mashtaka yoyote. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Mwakilishi Kombo ameachiwa baada ya majadiliano marefu yaliyohusisha maofisa wa upelelezi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba na viongozi wa ACT Wazalendo wakiongozwa na mwanasheria wa chama, Saleh Mohamed.

Taarifa za ndani zilizonaswa na MwanaHalisi Online, zimesema kuwa kilichowasukuma Polisi kumkamata Mwakilishi Kombo ni hofu na hatua ya kutumikia amri haramu za viongozi wa CCM.

“Wamejikuta hawana sababu ya kisheria ya kumshikilia. Kumkamata yenyewe hawakufuata utaratibu.

“Utaratibu unaelekeza unapotaka kumkamata mjumbe wa Baraza la Wawakilishi shuruti umuarifu Spika wa Baraza la Wawakilishi. Wamekwama walipoulizwa kama wamempa taarifa Spika, ilibidi waachane na fitna waloitenegeneza kwa kufuata amri haramu za wakubwa zao CCM,” amesema kiongozi mwandamizi wa ACT Wazalendo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Daniel Shilla hakupatikana kutoa maelezo kuhusu kukamatwa Kombo.

Hata hivyo, Ofisa wa ngazi ya juu ws Polisi Makao Makuu Mkoa mjini Wete amenukuliwa akisema, “hakuna mashtaka yoyote dhidi ya Mwakilishi unayeulizia kukamatwa kwake.”

Profesa Omar Fakih, mwakilishi wa Jimbo la Pandani na Mnadhimu wa wawakilishi wa upinzani Barazani amesema hatua ya kwanza aloichukua alipopata taarifa ya kukamatwa Kombo, ni kumjulisha Spika Zubeir Ali Maulid.

Jitihada za kumpata Spika ili kujua hatua alizochukua, zilishindikana. Mara kadhaa simu ilijibu haipatikani.

Mwakilishi Kombo alikamatwa akiwa Kituo cha Sizini, Wingwi, wakati akisaidiana na wananchi kudhibiti makundi ya watu wasiohusika waliopelekwa vituoni ili kuandikishwa.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesafirisha kwa meli vijana zaidi ya 1200 kuwapeleka kisiwani Pemba ambako uandikishaji wapigakura wapya ulianza Jumamosi.

Hatua hiyo ni muendelezo wa mikakati ya kusaidia CCM kupata watu wa kupiga kura Pemba kwa lengo la kuja kujitangazia ushindi kwenye uchaguzi.

Mtindo huo wa kupelekwa vijana waliosajiliwa kama vile kuajiriwa kwenye vikosi vya ulinzi vya SMZ na kufugwa kwenye kambi za vikosi hivyo, umezoeleka na ndio chimbuko la machafuko.

Mwaka 2004, watu wawili waliuliwa kwa risasi za moto zilizopigwa na askari wa serikali kufuatia mivutano ya wakati wananchi wenyeji wakizuia mamluki kuandikishwa vituoni Wilaya ya Mkoani.

Hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Mohamed Mahroun, alitangaza kwenye mkutano wa hadhara mjini Zanzibar kuwa vijana hawatakubali watu wasiohusika kujitokeza kwenye vituo kqa ajili ya kuandikishwa.

Uandikishaji wapigakura wapya utahamia Wilaya ya Wete, tarehe 5 Februari na kuingia Wilaya ya Chake Chake, baadaye Wilaya ya Mkoani ambako utakamilika Februari 22 na kuingia Unguja.

About The Author

error: Content is protected !!